NA KHAMIS AMANI

UPANDE wa mashitaka katika mahakama ya mkoa Vuga, umetakiwa kufuatilia jalada la kesi ya ubakaji inayomkabili Khamis Hemed Abdalla, ili kesi hiyo iweze kusikilizwa.

Amri hiyo imetolewa na Hakimu Hamisuu Saaduni Makanjira wa mahakama ya mkoa Vuga, baada ya upande wa mashitaka kudai kwamba hawajapokea jalada kutoka kituo cha Polisi husika.

Madai hayo uliyatoa wakati kesi hiyo ilipofikishwa mahakamani hapo kwa ajili ya kutajwa.

“Mheshimiwa shauri lipo kwa ajili ya kutajwa, upande wa mashitaka hatujapokea jalada, hivyo tunaomba shauri liahirishwe na kupangiwa tarehe nyengine kwa ajili ya kutajwa”, ulidai upande wa mashitaka, chini ya Wakili wa serikali Anuar Khamis Saaduni, kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP).

Upande wa utetezi chini ya Wakili wa kujitegemea Ruhaila Kassim, haukuwa na pingamizi na hoja hizo za upande wa mashitaka.

Katika kesi hiyo, Khamis Hemed Abdalla (25) mkaazi wa Kama Bondeni wilaya ya Magharibi ‘A’ Unguja, ameshitakiwa mahakamani hapo kwa makosa ya kutorosha na kubaka mtoto wa kike aliye chini ya uangalizi wa wazazi wake.

Machi 3, 2020 majira ya saa 10:30 za jioni huko Kama, bila ya halali alimtorosha msichana wa miaka (17) aliye chini ya uangalizi wa wazazi wake, kutoka Kama na kumpeleka kwenye banda la nyumba huko huko Kama, bila ya ridhaa kutoka kwa wazazi wake.

Mshitakiwa huyo alidaiwa kutenda kosa hilo kinyume na kifungu cha 113 (1) (a) cha sheria mamba 6/2016 sheria za Zanzibar.

Akiwa ndani ya banda hilo, kinyume na vifungu vya 108 (1) (2) (c) na 109 (1) vya sheria namba 6/2018, siku hiyo mshitakiwa huyo alidaiwa kumuingilia msichana huyo.