MOGADISHU, SOMALIA
VIONGOZI wa upinzani wa Somalia na majimbo ya mkoa wa Jubbaland na Puntland, pamoja na baraza la seneti la nchi hiyo, wamekataa uamuzi wa bunge wa kuongeza muda wa urais kwa miaka miwili.
Bunge dogo la Somalia juzi lilipiga kura kumuongezea muda rais Mohamed Abdullahi Farmajo wa kuwa madarakani kwa miaka miwili zaidi.
Hata hivyo uamuzi huo unapingwa na serikali ya jimbo la Jubbaland ambayo imetoa taarifa ikieleza kuwa hatua hiyo ya bunge ni kikwazo katika kujenga upya utawala wa nchi hiyo.
Msemaji wa rais wa Puntland, Sa’id Abdullahi Deni aliandika katika ukurasa wake wa twita akisema kuwa hatua hiyo iliyohukuliwa na bunge sio halali.
Naibu Spika wa Kwanza wa seneti ya Somalia Abshir Ahmed alihoji nguvu ya bunge dogo la Somalia kuchukua uamuzi huo mkubwa ambao unasababisha kuleta utatanishi kwa sababu hakuna idhini ya bunge la seneti.
Katika ukurasa wa twita waziri Mkuu wa zamani wa Somalia Hassan Ali Khaire alisema, rais atawajibika tu kwa kile kinachotokea au kitakachotokea baadaye katika nchi hiyo ya pembe ya Afrika.
Rais Farmajo alisifu uamuzi huo na kuwataka watu wa Somalia kutumia fursa hiyo na kushiriki katika mchakato wa kisiasa wa nchi hiyo.