NA MWANDISHI WETU

VIJANA wengi, wanawake na watu wenye ulemavu (PWDs) hawajafikiwa na huduma ya vitambulisho vya mzanzibari mkaazi (ZanID) kwa sababu ya urasimu uliopo katika shehia.

Hii ni kwa mujibu wa matokeo ya kampeni ya miezi mitano ya kutetea haki za vijana kupata ZANID, ilioendeshwa na asasi nne za kiraia zilizopo Zanzibar.

Vijana walio chini ya miaka 35 wanawakilisha idadi kubwa ya wananchi milioni 1.5 wa Zanzibar.

Katika taarifa yao kwa vyombo vya habari, asasi hizo ambazo ni Centre for Youth Dialogue (CYD), Jumuiya ya Wanawake Wenye Ulemavu Zanzibar (JUWAUZA), Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar (ZLSC) na Jumuiya ya Kupambana na Umaskini Pemba (PIRO), zilisema  kampeni hiyo ililenga kuwashirikisha vijana , wanawake na watu wenye lemavu kujadili changamoto juu ya upatikanaji wa ZanID hasa wakati wa mchakato wa maombi.

Matokeo yalionesha kuwa vijana wa vijijini hawakuwa na ufahamu mzuri na taratibu za maombi na walikosa nyaraka zinazohitajika ikiwa ni pamoja na vyeti vya kuzaliwa sawa na wanawake wanaoishi na ulemavu.

“Viziwi walikabiliwa na ugumu wa kupata habari sahihi juu ya mchakato wa maombi ya ZanID kwa sababu ya vizuizi vya mawasiliano,” ilisema taarifa ya pamoja ya asasi hizo.

“Tumewasilisha changamoto na mapendekezo yaliyoainishwa kwa wadau muhimu wa ZanID. Wote wamekubali kushirikiana na kusaidia asasi zetu kufanya kazi katika kuboresha upatikanaji wa ZanID hasa kwa makundi aliyojumuishwa,” iliongeza taarifa hiyo.

Asasi hizo zilitoa wito kwa wadau kuingilia kati na kuanzisha mabadiliko ya sera juu ya suala hilo na kujibu changamoto zilizoanishwa ili kuimarisha ufikiaji wa vijana katika kupata ZanID.

“Tunasisitiza kwa wadau na wahusika wengine kupata suluhisho la kudumu la shida hii na kujitolea kusaidia vijana, wanawake na watu wenye ulemavu kupata ZanID ili kufikia huduma za kijamii na kiuchumi,” ilisema taarifa hiyo.