NA KHAMISUU ABDALLAH

BAADA ya upande wa mashitaka kushindwa kuthibitisha kosa dhidi ya mfanyakazi wa hoteli ya Protea hatimae Mahakama ya Wilaya Mwanakwerekwe imeifuta kesi inayomkabili mshitakiwa huyo.

Akisoma Hukumu hiyo, Hakimu Asya Abdalla Ali, alisema pamoja na upande wa mashitaka kuwasilisha mashahidi wanne mahakamani hapo, lakini ushahidi wao una mashaka kutokana na kutofautiana, hivyo mahakama inamuachia huru mshitakiwa huyo chini ya kifungu cha 219 cha sheria namba 7 ya mwaka 2004 sheria za Zanzibar.

Mahakama pia ilitoa haki ya rufaa kwa siku 30 kwa mtu asiridhika na hukumu hiyo.

Aliyeachiwa huru ni Omar Kombo Mfundo (43), mkaazi wa Bububu Wilaya ya Magharibi ‘A’ Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.

Awali kesi hiyo ilipofunguliwa mahakamani hapo Agosti 23 mwaka 2018, ilidaiwa na Mwendesha Mashitaka Wakili wa serikali kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Nyasi Haji Kombo ,alidai kuwa mshitakiwa huyo alipatikana na kosa la wizi baada ya kuaminiwa kinyume na kifungu cha 274 (7) (b) cha sheria namba 6 ya mwaka 2004 sheria za Zanzibar.

Ilidaiwa kuwa mnamo mwaka 2015, nyakati tofauti huko Mazizini katika hoteli ya Protea, mshitakiwa huyo akiwa mhasibu wa hoteli hiyo aliaminiwa kwa kuzihifadhi fedha benki kwa ajili ya kulipa wafanyakazi na kufanya matumizi kwa ajili ya hoteli badala yake aliiba fedha taslimu shilingi 3,987,000 mali ya hoteli hiyo kitendo ambacho ni kosa kisheria.