NA HAFSA GOLO
SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar imepongezwa kwa kuandaa mfumo bora wa kuenzi fikra na mchango wa maendeleo nchini uliotekelezwa na viongozi wakuu wa kitaifa.
Imeelezwa kwamba hatua hiyo itakuwa ni moja ya sehemu ya utoaji elimu ya historia ya Zanzibar kwa vizazi vya sasa na baadae.
Wananchi mbali mbali waliyasema hayo kwa nyakati tofauti walipokua wakizungumza na gazeti hili, Mkwajuni mara baada ya kukamilika kwa zoezi la dua ya eliekuwa Waziri wa Kiongozi wa kwanza wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Bregedia Jeneral Ramadhan Haji Faki.
Mmoja wa wananchi hao, aliejitambulisha kwa jina la Patima Haji (57) alisema uthubutu wa serikali wa kuweka sheria maalumu ya kuwaenzi viongozi wakuu wa kitaifa utasaidia kuleta hisia na kupanua wigo kwa vijana juu ya umuhimu wa kuheshimu viongozi sambamba na kulinda tamaduni na historia.
“Utaratibu wa serikali kwa kila mwaka kuzuru makaburi ya viongozi wakuu katika maeneo miji mbali mbali itaibua hamasa na ari mpya kwa vijana yakutaka kuelewa kiongozi namna alivyolitumikia nchi,jambo ambali litasaidia kuifahamu historia ya nchi yao”,alisema.
Nae Ramadhan Haji (61) mkaazi wa Matemwe alisema, kutokana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia ipo haja kwa serikali kuongeza juhudi zaidi katika kuandaa mifumo madhubuti ambayo itaimarisha nguzo imara kwa vijana wa sasa na baadae.
Alisema kufanya hivyo kutasaidia kudhibiti na kufuata misingi mema ilioasisiwa na viongozi wakuu hasa katika suala zima la kujitolea katika ujenzi wa taifa.
“Nchi yoyote ili iweze kupiga hatua ya maendeleo inahitaji nguvu kazi ya vijana hivyo juhudi na fikra sahihi za serikali zinazoendelea kuchukuliwa na watendaji wakiwa wabunifu katika kuisaidia serikali juu ya namna bora ya kudhibiti kumbukumbu na kuelimisha vizazi vipya kuhusu michango ya maendeleo iliyotolewa na waasisi bila ya shaka Zanzibar itakuwa na mabadiliko ya kijamii na kiuchumi katika muda mfupi”,alisema.
Miongoni mwa vijana walioshiriki katika dua hiyo ambae ni mwanafunzi wa Skuli ya Mkwajuni Ali Fumu alisema,mfumo wa serikali wa kuandaa dua maalumu kila inapofika mwezi Aprili inawasaidia kufahamu historia ya viongozi ambao walisaidia kuleta maendeleo ya nchi yetu.
“Kitendo kama hichi kimetupa faraja sisi vijana kwani viongozi wengine hatuwajui lakini hapa tunapata historia zao na kujifunza mengi ambayo yatasaidia kuendeleza maendeleo ya nchi yetu”,alisema.