NA ASIA MWALIM

KAMATI za wananchi zilizo pewa dhamana ya kusimamia miradi ya kimaendeo katika Jimbo zimetakiwa kuweka utaratibu wa kusaidana yanapotokea matatizo, Ili kuhakikisha wanatoa huduma nzuri kwa wananchi.

Mwenyekiti wa Kamati ya huduma za jamii, ambae pia ni Diwani wa kuteuliwa Manispaa Magharibi ‘B’, Thuwaiba Jeni Pandu, aliyasema hayo katika ziara yake ya kusikiliza kero zinazo wakabili wananchi wa shehia ya Pangawe Wilaya ya Magharibi ‘B’ Unguja.

Alisema ni vyema viongozi waliopewa dhamana ya kusimamia wananchi wa Wilaya hiyo kufanya kazi kwa bidii ikiwemo kufuatilia na kutatufa ufumbuzi wa matatizo yaliowazunguka.

Aidha, aliwataka viongozi wa kamati hiyo kufanya kazi kwa mashirikiano, ili kuhakikisha wanatatua mahitaji ya wananchi bila ya kuweka ubaguzi wa aina yoyote kama sheria inavyoeleza.

Amesema lengo la kufanya ziara hiyo ni kutoa ufumbuzi unaofaa, baada kupokea malalamiko mengi kutoka kwa wananchi kukosa maji kwa muda mrefu, na kulazimika kutumia gharama nyingi kununua maji.

Alifahamisha kuwa katika awamu iliyopita viongozi wa jimbo hilo wamefanikiwa kuchimba visima vingi, ili kuhakikisha wanamaliza tatizo la maji maeneo hayo, hivyo wanapaswa kuweka utaratibu wa kutumia visima hivyo.

Alieleza kuwa Serekali ya Mapinduzi ya Zanzibar ipo mstari wa mbele katika kuwatumikia wananchi wake, waliamua kuboresha huduma hiyo ambayo ipo chini ya usimamizi wa kamati, hivyo waweke utaratibu mzuri.

“Kwa kweli katika eneo hili visima vipo na maji yapo isipokuwa utaratibu unaotumika hapa ndio mbovu” alisema.

Aidha, amewataka wananchi wa shehia hiyo kuwa nasubira katika kipindi hichi, kwani viongozi wa jimbo hilo wapo makini, ili kuhakikisha tatizo hilo linaweza kumaliza kwa haraka ili waendeleee kupata huduma hiyo kama awali. 

Sambamba na hayo amesema viongozi wamekua wakijitahidi kuhakikisha wanaondosha changamato mbalimbali ikiwa ni pamoja na kujenga visima, hivyo ni vyema kwa wanakamati kuwajibika ipasavyo ili kuondoa usumbufu wanaoupata wananchi.

Nao wanakamati wamesema tatizo kubwa lilokuwepo baadhi ya wananchi kushindwa kulipa ada, ambayo inatumika kununua umeme, pia kushindwa kushindwa kufanya matengenezo pale linapo tokezea tatizo.

“Wananchi wengi wananshindwa kulipia ada ya maji, hali ambayo linapotokea tatizo dogo tu tunashindwa kulitatua wenyewe” alisema.

Kwa upande wa wanachi wa shehia hiyo walimpongeza mwenyekiti huyo kwa ujio wake, wa kujali kusikiliza changamoto zinazowakumba wananchi, jambo ambalo limewapa matumaini.