NA NASRA MANZI

VIONGOZI wa Baraza la Vijana wilaya ya Mjini waliochaguliwa kuliongoza   baraza hilo wameahidi kushirikiana na serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kukabiliana na changamoto zinazowakabili vijana hapa nchini.

Wakizungumza mara baada ya kumalizika kwa mkutano mkuu wa uchaguzi, uliofanyika katika ukumbi wa studio za muziki na filamu huko Rahaleo, viongozi hao wapya walisema kwa kushirikiana na serikali ndipo kutakakofanikisha utatuzi wa changamoto za vijana hapa nchini.

Walisema watahakikisha kutoa ushirikiano ili kuleta ufanisi utakaoleta maendeleo katika Wilaya na kuondosha changamoto kwa Vijana.

Aidha walisema vipaumbele watakavyovitekeleza kutoa ajira kwa vijana ikiwemo fursa za kitalii.

Akisoma taarifa fupi mara baada ya kumkaribisha mgeni rasmi Ofisa wa Vijana Amina Salum Ali, alisema lengo la baraza hilo ni kuwajenga vijana kutambua utaifa wao ili kuongeza uzalendo na imani ya kuipenda nchi yao.

Alisema ili kuimarisha mabaraza ya vijana, serikali italazimika kutengeneza mbinu zitakazoleta ufanisi katika kuhakikisha wanaendelea kupewa kipaumbele kwenye mipango na fursa mbalimbali.

Akifungua mkutano mkuu wa baraza la vijana wilaya Mjini, mkuu wa wilaya hiyo Rashid Simai Msaraka, alisema uchaguzi usiwajengee vijana misingi ya uhasama bali hiyo ndiyo changamoto ya demokrasia.

“Kama umeshindwa katika uchaguzi huna sababu ya kujenga misingi ya uhasama shirikiana na aliyeshindwa kwa ajili ya maendeleo ya nchi na hiyo ndio demokrasia”, alisema mkuu huyo.

Mkuu huyo aliwataka viongozi walioshinda kuhakikisha wanakwenda kusimamia ajenda na miradi ya vijana ili rika hilo kubwa hapa nchini liweze kuepukana na changamoto zinazowakabili.

Msaraka aliwaomba vijana kuhakikisha wanashirikiana na serikali hasa ikizingatiwa kuwa wana umuhimu mkubwa kama nguvu kazi ya uzalishaji na kuinua uchumi.

Katika mkutano huo, kamati ya uchaguzi taifa ilitangaza matokeo ya uchaguzi kwa Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti, wajumbe watakaowakilisha Taifa na   wajumbe watatu watakaowakilisha Baraza Taifa.

Aliyeshinda nafasi ya mwenyekiti ni Salmini Mussa Nahodha wa Baraza la Vijana Wilaya Mjini aliyepata kura 50 sawa na asilimia 80.64, huku Makamu Mwenyekiti Zainab Hassan Omar aliyepata kura 46 sawa na asilimia 74.19