NA MWAJUMA JUMA

LEO Aprili 28, ni siku ya Usalama na Afya Kazini, ambapo kwa Zanzibar maadhimisho hayo yalifanyika jana ambapo Idara ya Usalama na Afya Kazini ilitoa mafunzo juu ya usalama.

Mafunzo hayo yaliwashirikisha wanafunzi wa vyuo vikuu kuwapa elimu juu ya usalama wa afya kazini.

Siku hii imewekwa maalumu na Shirika la Kazi Duniani (ILO) ili kuhamasisha kujikinga na ajali pamoja na maradhi yatokanayo na sehemu za kazi.

Pamoja na mambo mengine lakini lengo hasa lililokusudiwa ni kwa waajiri, wafanyakazi wa taasisi za umma na wa Serikali, kuelimisha jamii juu ya umuhimu wa usalama na afya na mabadiliko yanayotokea katika sehemu za kazi.

Akizungumza katika mafunzo hayo, Afisa Mkaguzi Usalama Kazini Said Bakari alisema lengo la kutoa elimu hiyo kwa wanafunzi wa vyuo vikuu ni kuwaandaa wanafunzi hao ambao baadae watakuwa waajiriwa ili kujua juu ya usalama wao wanapokuwa makazini.

Hivyo alizitaka Taasisi za elimu na kijamii, kuweka miundombinu rafiki itakayowezesha usalama wa watumiaji wake pindi yanapotokea majanga.

Bakari alieleza kuwa wanatakiwa kutilia mkazo suala la ubunifu wakati wanapobuni na kutengeneza miundombinu ya majengo kama vile milango na madirisha kwenye majengo na sehemu za mikusanyiko ikiwemo skuli.

Aidha alisema suala la uwepo wa madirisha yenye kutoa mwangaza mkubwa katika majengo yenye mikusanyiko ya watu wengi ni bora kwa kuwa kunawaweka watu hao katika hali ya usalama zaidi na kujikinga na maradhi.

Alisema katika utafiti walioufanya wamegunduwa wanafunzi wengi wa madara ya chini kuanzia la tatu na kuendelea wamekuwa na uoni hafifu kunakochangiwa na kukosa mwangaza katika skuli wanazosoma.

Hivyo wao wakiwa ni wategemezi wa kada mbalimbali hapo baadae, Afisa huyo aliwataka wajenzi wanapokuwa katika hatua ya mwanzo ya ujenzi ya ukadiriaji wa majengo wasiruhusu kuwepo madirisha madogo kwa kuwa yanaweza kuleta athari hapo baadae.

“Kuna baadhi ya walimu huyaziba kwa kuhofia utoro au kupigwa mawe, kudhibiti utoro wa wanafunzi na kusahahu kwamba wanapofanya hivyo wanawaingiza katika matatizo wanafunzi ambao wengi wao sasa wanatumia miwani kutokana kukosa mwanga madarasani,” alisema.

Alisema ili kuepukana na hali hiyo ni vyema kukaandaliwa njia mbadala ya kudhibiti utoro maskulini na sio kuzibwa madirisha na milango ambayo inatakiwa iwe inafunguka kwa nje ili linapotokea tatizo iwe rahisi kufunguka.

“Itakumbukwa mwaka mmoja kulitokea moto katika bweni la skuli mkoani Tabora Tanzania Bara. Wakati moto huo ulipozimwa yalikutikana mafuvu ya vichwa chini ya mlango, ambao uhalisia wake walionekana wote walitaka kupita pale lakini hawakuweza kujiokoa kutokana na miundombinu ya mlango huo kutokuwa rafiki kwao,” alisema Said.

Nae Afisa  Msajili Mkaguzi wa Sehemu za Kazi kutoka kitengo hicho, Ame Faki Salum, alisema kuwekeza katika usalama na afya kazini ni gharama iliyowazi ambayo faida yake ni kubwa iliyojificha.

“Unapowekeza tambua unamuweka mfanyakazi wako awe na afya, kuwa katika sehemu salama, vifaa vinavyofanya kazi vizuri na kudumu kwa muda mrefu na kuzalisha kilichobora”, alisema.

Sambamba na hayo alisema kuwa wengi wa vijana wanapoajiriwa malengo yao makubwa ni kuweza kupata mshahara na kuwa na mali nyingi na kusahahu juu ya afya na usalama wao wanapokuwa makazini jambo ambalo iwapo hawakufanikiwa kukabiliwa na msongo wa mawazo unaochangia kupata ugonjwa ambao kutibika kwake unakuwa mgumu.

FAIDA ZA KUDHIBITI MATUKIO YA AJALI NA MARADHI KWENYE SEHEMU ZA KAZI

Kupunguza muda unaopotea kutokana na maradhi au ajali, Kupunguza madhara na maumivu kwa wafanyakazi na jamii ni miongoni mwa faida.

Faida nyengine ni Kupunguza gharama za matibabu na huduma kwa wafanyakazi wasiokuja kazini au fidia kwa jamii, Kuondoa uwezekano wa kulipa wafanyakazi wengine ili wafanye kazi ya wale waliopata ajali au walikuwa wagonjwa.

Kupunguza gharama za uchunguzi wa ajali, kupunguza muda wa kusimamisha uzalishaji ili kuhudumia majeruhi au wagonjwa, kupunguza muda na gharama za malipo ya fidia kwa wafanyakazi walioumia au jamii iliyoathirika na kuongeza mori ya wafanyakazi na kuzalisha zaidi.

HATUA ZA KUCHUKUWA ILI KUJIKINGA

Kuifahamu hatari yenyewe kwa kujua inatokana na nini na namna inavyoweza kudhibitiwa kwa kuondolewa kabisa, au kutenga na kupunguza makali.

Hatua nyengine ni kujua cha kufanya kama hatari itatokea (udhibiti wake, kama vile nani apewe taarifa na kwa njia gani na pia wafanyakazi wenyewe waweze kutambuwa taathira ya matendo yao na ya wafanyakazi wenzao, wateja, watoa huduma kutoka nje.

MAMBO YANAYOHITAJIKA KWENYE SEHEMU ZA KAZI KWA AJILI YA USALAMA NA AFYA KAZINI

Ili kuwepo na usalama wa afya kwa wafanyakazi wake ni lazima kuwepo na mwanga mkubwa, mzunguko mzuri wa hewa yenye ubora unaotakiwa, hali ya hewa nzuri, isiokuwa na joto wala baridi sana.

Aidha uwepo wa usafiri, vifaa vya kutosha vya usalama na kukabili hali ya dharura kama kuwepo na kifaa cha kuzimia moto, kifaa cha huduma ya kwanza na paa imara lisilovujisha maji wakati wa mvua.

VYANZO VYA HATARI KWENYE SEHEMU ZA KAZI

Miongoni mwa hatari sehemu za kazi hutokana na vyanzo tofauti, ikiwemo sehemu yenyewe ya kazi, aina ya kazi ambayo inafanyika, mitambo na zana zinazotumika, vifaa vinavyotumika, kemikali zinazotumika na mali ghafi inayotumika.

TAHADHARI

Zipo baadhi ya athari zinazotokana na sehemu za kazi zinazoweza kuonekana mara moja wakati zinapoanza kwa ghafla ambapo nyingi zao zinakuwa zinachelewa kuonekana na kuchukuwa miaka mingi mpaka kufikia kujitokeza.

Hivyo basi ni vyema kufanya uchunguzi wa afya za wafanyakzi kila baada ya vipindi maalumu au inapotokea dharura.

Miongoni mwa baadhi ya athari zinazopatikana katika sehemu za kazi ni kupata maambukizi ya maradhi yenye kuambukizika, kupoteza uwezo wa kuona kutokana na mwanga kuwa mdogo sana au mkubwa sana, kupoteza uwezo wa kusikia kutokana na kelele, kupoteza uwezo wa kuhisi harufu na kupotea uwezo wa kuhisi ladha.

Kauli mbiu ya siku ya Kimataifa ya Usalama na Afya Kazini kwa mwaka huu 2021 ni  ‘Tarajia kujitayarisha na kukabiliana na matatizo yoyote yasiyokuwa ya kawaida –wekeza sasa kwenye mifumo inayohimili vyema masuala ya usalama na afya kazini’