NA ABOUD MAHMOUD

WABUNGE na Wawakilishi wa majimbo mbali mbali kisiwani Unguja wameshauriwa kuiga mfumo unaotumiwa na viongozi wa Jimbo la Kikwajuni katika kuandaa mashindano ya soka kila inapofika mwezi wa Ramadhan.

Hayo yamesemwa na wadau wa soka visiwani humu walipokutana na mwandishi wa habari hizi mara baada ya uzinduzi wa michuano iliyopewa jina la Masauni Jazeera Cup.

Wadau hao walisema wamekua wakifuatilia mashindano hayo kila mwaka kutokana na kuongeza hamasa ya mchezo huo hususan katika kipindi hichi cha mwezi mtukufu.

“Nawashauri wabunge na wawakilishi wa majimbo mengine waige mfano wa Masauni na Jazzera katika kuandaa mashindano kama haya, ili wananchi waweze kufurahi zaidi,”alisema Omar Kombo.

Omar alifahamisha kuwa kutokana na kushuka hadhi ya soka visiwani humu na mashindano mbali mbali, kusimamishwa katika kipindi hichi ikiwemo ligi kuu ni vyema viongozi hao wa majimbo, kuwaunganisha vijana katika kudumisha na kuongeza hadhi ya michezo nchini.

Nae Tariq Himid mdau wa soka kutoka Jimbo la Kiembesamaki alisema kila inapofika mwezi wa Ramadhani, hushiriki kutizama mechi kutoka timu mbali mbali za Kikwajuni ili kupata burudani za vijana hao.

“Kila yanapoandaliwa mashindano haya mimi nahudhuria na sababu kubwa inayonifanya nije ni kutizama vipaji walivyokuwa navyo vijana wetu hapa Unguja na napenda sana katika jimbo letu wafanye kitu kama hichi ili kuboresha na kupandisha hadhi ya soka,”alisema Tariq.

Sambamba na hayo mdau mwengine wa soka Raya Othman kutoka jimbo la Kwahani alisema ni vyema viongozi wa majimbo kuiga mfano huo kwani itasaidia kuleta hamasa zaidi na baadae kuandaliwa mashindano ya majimbo.

Mashindano ya kuwani kombe la Masauni na Jazeera katika Jimbo la Kikwajuni ni miongoni mwa mashindano pekee makubwa yanayofanyika kila mwaka katika mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani.