TRIPOLI, LIBYA
RAIS wa Baraza la mpito nchini Libya, Mohammad Menfi, amewaachia huru wafungwa zaidi ya 100 ambao walikuwa wanapigana na jeshi lenye makao makuu yake mashariki karibu na mji mkuu Tripoli.
Wafungwa hao walizuiliwa katika mji wa Zawiya, ulioko kilomita 45 magharibi mwa Tripoli, na vikosi vilivyoshirikiana na Serikali ya zamani ya Mkataba wa Kitaifa inayoungwa mkono na Umoja wa mataifa.
“Tumekubali kuachia huru wafungwa kufuatia kamati ya mazungumzo ya mji wa Zawiya, ambayo inachukuliwa kuwa hatua muhimu kuelekea maridhiano ya kitaifa ambayo Baraza la Urais lilizindua wakati wa kupokea ofisi,” Menfi.
Menfi alithibitisha kuwa Baraza la Urais linataka kuwaweka pamoja Walibya na kumaliza hali ya mgawanyiko nchini.
Pia alitaka “kujumuisha maadili ya msamaha na uvumilivu kwa kutanguliza maslahi ya kitaifa ya Libya.”
Watu, familia na ndugu na jamaa waliwalaki jamaa zao wakati wakiachiliwa huru kutoka magereza mbalimbali mjini Tripoli.
Jeshi lenye makao yake mashariki lilikuwa limeanzisha mashambulio ya kijeshi dhidi ya serikali ya zamani iliyoungwa mkono na Umoja wa Mataifa, ambayo ilidumu kwa zaidi ya mwaka mmoja na kumalizika mnamo Juni 2020 na kuondolewa kwa jeshi lenye makao yake mashariki mwa nchi hiyo.