BUSIA, UGANDA

WAFANYABIASHARA nchini Uganda wanaingiza shehena za tani za mahindi nchini Kenya kwa njia ya magendo.

Hatua hiyo imekuja kufuatia, Kenya kupiga marufuku wafanyabishara kuingiza mahindi nchini humo kutoka Uganda.

Kwa mujibu wa taarifa, wafanyabishara wengi wanaingiza mahindi nchini Kenya kwa njia ya magendo wakipitia kwenye mipaka iliyopo mji wa Busia na kuendelea na biashara yao kama kawaida.

Miongoni mwa maeneo ambayo wafanyabishara hao wanapitisha mahindi kwa njia ya magendo na kwenda kuuza nchini Kenya ni pamoja na Sofia, Marachi, Buteba, Buhehe, Lumino, Majanji, Busime na Masinya.

Mwenyekiti wa wafanyabishara wa mipakani nchini Kenya, David Erulu, alisema kwa sasa kuna wafanyabiashara wengi kutoka Uganda wanaoingiza mahindi nchini Kenya kwa njia ya magendo.

Alisema Kenya ina uhaba mkubwa wa mahindi na imechangiwa kutokana na vikwazo ilivyoviweka kwa kuzuia mahindi nchini humo huku pia kukiwa na mahitaji makubwa.

“Kenya ina uhaba wa mahindi na maeneo ya Kericho na Kitale viwanda vya kukoboa unga wa mahindi vimeishiwa na hifadhi kwenye maghala yao”, alisema David Erulu.

Erulu alisema wananchi wengi wa Kenya wanategemea unga wa mahindi kwa ajili ya chakula ikiwemo chakula mashuhuri kinachojulikana kama kwete.