TRIPOL, LIBYA
JUMLA ya wahamiaji haramu 138 waliokolewa na Walinzi wa Pwani ya Libya kutoka pwani ya magharibi mwa nchi hiyo, Jeshi la Wanamaji la Libya limesema hapo jana.
Taarifa zilisema kuwa wahamiaji hao ni kutoka mataifa tofauti ya Afrika, ambao waliokolewa na jeshi la Wanamaji la Libya na kuplekwa katika mji mkuu wa Tripoli Naval Base.
Mamia ya wahamiaji haramu wameokolewa na kurejeshwa Libya katika siku chache zilizopita, jeshi la wanamaji la Libya liliongeza.
Libya imekuwa mahali ambapo hutumiwa wahamiaji haramu ambao hujaribu kuvuka Bahari ya Mediterania kwenda barani Ulaya hasa tangu kuangushwa kwa utawala wa kiongozi wa Libya Muammar Gaddafi mnamo mwaka 2011.
Mnamo mwaka wa 2020, jumla ya wahamiaji haramu 11,891 waliokolewa na kurejeshwa Libya, Shirika la Kimataifa la Uhamiaji limesema kuwa wahamiaji 381 walifariki na 597 walipotea katikati ya bahari ya Mediterranea wakati wakivuka kuelekea Ulaya.
Aidha taarifa zilisema kuwa wahamiaji waliookolewa huishia ndani ya vituo vya mapokezi vilivyojaa watu kote Libya, licha ya wito wa mara kwa mara wa kimataifa wa kufunga vituo hivyo.