NA MWANDISHI WETU

NAIBU Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara, ametoa siku 14 kwa uongozi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), kumpa taarifa ya mradi wa upanuzi wa Bandari ya Tanga unaogharimu zaidi ya shilingi Bilioni 500.

Hatua hiyo imefikiwa baada ya Naibu Waziri huyo kutoridhishwa na maelezo ya namna kiasi cha shilingi Bilioni 172 zilivyotumika katika ujenzi wa kuongeza kina katika bandari hiyo ili kuziwezesha meli kubwa kutia nanga.

“Natoa siku 14 niwe nimepata taarifa ya kina kuhusu mradi huu na namna ya mchakato wa kumpata mkandarasi ulivyofanyika, nani alifanya upembuzi yakinifu, nani alishauri kutumiwa kwa hizo fedha, nani walihusika katika usimamizi wa huo mradi na tathimini ya fedha zilivyotumika ili kuiwezesha Serikali kuchukua hatua”, amesisitiza Naibu Waziri Waitara.

Amesema nia ya Serikali ni kuiona Bandari ya Tanga ikifanya kazi katika viwango vya juu na hivyo kuchangia kukuza uchumi wa Taifa na yoyote atakayebainika kukwamisha dhamira hiyo ya Serikali atachukuliwa hatua kali.

Amemtaka Mkurugenzi Mpya wa TPA, kupanga safu yake ya uongozi mapema iwezekanavyo, ili kuendana na kasi na matarajio ya Serikali ya Awamu ya Sita.

Amewataka watumishi wa Taasisi zote zilizo chini ya Wizara yake kusoma mpango wa Maendeleo ya Taifa wa 2020/ 2025, ili kuweza kujua wanatakiwa wafanyeje na kwa namna gani katika kipindi hicho.

Wakati huo huo,  Waitara, amewaonya wakandarasi na wafanyakazi wababaishaji na wanaoidanganya Serikali kuwa wana sifa na vigezo, lakini wanajenga barabara na madaraja chini ya viwango  kuacha tabia hiyo mara moja, kwani husababisha gharama kubwa kwa Serikali kutokana na kufanya matengenezo ya barabara mara kwa mara.

Naibu Waziri Mwita ametoa kauli hiyo jijini Dodoma, katika kikao kazi na menejimenti na wafanyakazi wa Bodi ya Mfuko wa Barabara na kupokea taarifa ya Bodi hiyo.

Naibu huyo ameupongeza mfuko huo kwa namna unavyoweza kusimamia matengenezo ya barabara nchi nzima kwa uharaka unaoendelea kufanywa na Wakala wa Barabara  (TANROADS) pamoja na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA).

Amezungumzia umuhimu wa wafanyakazi kutoa elimu sahihi kwa jamii, ili kuilinda  miundombinu yote ya Barabara, Madaraja, Reli, Bandari, Vivuko na Viwanja vya Ndege ili idumu kwa muda mrefu.

“Tutahakikisha tunachujana humu humu ndani na ukigundua kuwa wewe sio mwenzetu ujitafakari mapema kabla sijakufikia, tunahitaji watumishi wazalendo na wakandarasi wenye sifa na weledi sio wababaishaji”, amesisitiza Naibu Waziri huyo.

Katika hatua nyengine, Naibu Waziri Waitara, amemtaka Mkandarasi Power Construction Corporation ya China, Msimamzi wa mradi Intercontinetal Consultants and Tecnocrtrats Pvt ya India  kwa kushirikiana na Apex Engineering Co. ya Tanzania na Meneja wa TANROADS Mkoa kuongeza vifaa na wafanyakazi ili kazi ikamilike kama ilivyopangwa na kusisitiza kwamba Serikali itaendelea kumlipa mkandarasi kwa wakati.

Aidha amewataka wafanyakazi wanaojenga daraja hilo kufanya kazi kwa uzalendo, bidii na kujifunza, ili kuwezesha Taifa kuwa na wataalam wake wa madaraja makubwa siku zijazo.

Akikagua maendeleo ya ujenzi wa barabara ya Tanga – Pangani (KM 50) kwa kiwango cha lami, Naibu huyo alimtaka mkandarasi M/S China Henan International kukamilisha barabara hiyo kwa wakati na Serikali haitakubali visingizio visivyo na tija.

Akizungumza mara baada ya ukaguzi huo, Naibu Waziri Waitara amesema ujenzi wa Daraja jipya la Wami ni mkakati wa Serikali katika kuongeza ufanisi katika barabara ya Chalinze – Segera na kupunguza adha kwa abiria na wasafirishaji wanaotumia daraja la zamani lenye urefu wa mita 88.75.

“Kutokana na umuhimu wa daraja hili Serikali imeamua kujenga daraja jipya ili kuondoa adha katika daraja la zamani lililojengwa mwaka 1959 kutokana na kutokidhi mahitaji ya magari yanayopita kwa sasa, kuwa jembamba na lenye njia moja na barabara zake unganishi kupita katika miinuko mikali na kona mbaya na hivyo kusababisha ajali za mara kwa mara”, amesema Naibu Waziri huyo.

Nae, Mkurugenzi wa TPA, Erick Hamis, amesisitiza kwamba taarifa zinazotakiwa zitawasilishwa kwa wakati na miradi inayoendelea katika Bandari ya Tanga itakamilika katika kipindi cha miaka mitatu ijayo ili kuiwezesha Bandari hiyo kuhudumia tani milioni mbili za shehena toka tani laki saba zinazohudumiwa kwa sasa.

“Tutahakikisha uwepo wa reli na barabara za uhakika katika Mkoa wa Tanga kuelekea mikoa ya Kaskazini na katikati ya nchi kunawezesha bandari hii kufanya kazi kwa ufanisi”, amesema Hamis.

Naye, Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Mkoa wa Tanga, Mhandisi Alfred Ndumbaro, amesema Serikali imetoa kiasi cha shilingi Bilioni 4 kwa ajili ya kulipa fidia  wananchi waliopisha ujenzi wa barabara hiyo na zoezi la kulipa fidia litaanza Mei 03, mwaka huu.

Upande wa Meneja  wa Wakala wa Barabara (TANROADS), Mkoa wa Pwani, Mhandisi Yudas Msangi, amesema Daraja jipya la Wami lenye urefu wa mita 510 na barabara unganishi zenye urefu wa kilometa 3.8 linalounganisha miji ya Chalinze – Pwani na Segera – Tanga litakamilika mwezi Septemba mwaka huu.

Mhandisi Msangi, amemueleza Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara, mkoani Pwani wakati alipokagua maendeleo ya ujenzi huo uliofikia asilimia 50.5 na kumuahidi kuwa kazi itakamilika kama ilivyopangwa.

Zaidi ya shilingi bilioni 67 zinatarajiwa kutumika katika ujenzi wa Daraja jipya la Wami lenye urefu wa mita 510 na upana wa mita 11.85 ambalo limezingatia sehemu ya barabara za magari, watembea kwa miguu na vizuizi kwa ajili ya usalama hivyo linatarajiwa kupunguza ajali katika eneo la Mto Wami na kuhuisha huduma za usafiri na uchukuzi katika barabara kuu ya Chalinze – Segera.