NA MWANAJUMA MMANGA

JUMUIYA ya Wakimbiza Mwenge wa Uhuru Kitaifa (TAUTA) umetoa pole kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, kutokana na kifo cha aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Magufuli, aliyefariki Machi 17 mwaka huu.

Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Meja Mstaafu wa Jeshi la kujenga Uchumi (JKU), Abubakar Saleh Juma, alisema hayo wakati akizungumza na mwandishi wa gazeti hili jana na kutoa pole hizo kwa Watanzania na familia ya marehemu Dk. Magufuli aliyeezikwa Machi 26, mwaka huu.

Abubakari alisema Jemedari Magufuli alikuwa mstari wa mbele kulinda falsafa ya hayati baba wa taifa la Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, hasa kwa dhana yake aliyoitoa kwa Watanzania kuwa watawasha mwenge na kuweka juu ya mlima Kilimanjaro.

Aidha alisema falsafa hiyo ya hayati Magufuli alitekeleza kwa vitendo na kuiyenzi, kusimamia mbio za mwenge zinakwenda kama azma ya baba wa taifa ya Mwalimu Nyerere.

“Kamwe hatutowasahau hayati Mwalimu Nyerere na Magufuli kwa ushupavu wao wa kuwatetea Watanzania sambamba na kupigania nchi,” alisema.

Alisema Marehemu Magufuli alikuwa ni kiongozi shupavu na mchapakazi, mwenye msimamo, mtetezi wa wanyonge na wafanyabiashara wadogo wadogo (wamachinga) hivyo viongozi waliobakia wanapaswa kufiuata nyayo zake.

“Dk. Magufuli alikuwa akipiga vita rushwa, uzembe, wizi na ubadhirifu wa mali za umma na za serikali hivyo ipo haja ya kuendelea kuyasimamia mambo hayo,” aliongeza Mwenyekiti huyo.

Aidha alimuomba mjane wa Marehemu Magufuli, mama Janet Magufuli na familia kuwa na subra katika kipindi  kigumu na kumtaka kuwa na uvumilivu na kumuo,mbea kwa Mwenyezi Mungu nguvu ya kumuombea dua mume wake na kuwaongoza vyema watoto.

Nae Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wakimbiza Mwenge wa Uhuru Kanda ya Zanzibar, Khamis Mbaraka Abdalla, alisema Magufuli watamkumbuka milele kwa kile alichokifanya kwa watanzania na walikuwa wamepanga mabo mengi kutekelezewa katika Mwenge wa uhuru kamwe  hatutomsahau tena.

“Tunaimani na Rais aliechaguliwa kushika nafasi hiyo Mama Samia na tunampa hongera mwanamama huyo kumtaka kufata nyayo ya marehemu Magufuli yale yote aliyoyaacha ikiwemo kulinda uhuru wa watanzania,” alisema.

Alisema marehemu Magufuli alikuwa na malengo makubwa ya kuifikisha Tanzania kwenye uchumi wa viwanda na uchumi wa kati wa kiwango cha juu.