NA HAJI NASSOR

WANAWAKE waliogombea nafasi za ubunge na uwakilishi kisiwani hapa, wameitaka Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu wa Uchumi Zanzibar (ZAECA) kujipanga vyema kwenye uchaguzi mkuu mkuu ujao ili kuwakamata wagombea wanaume wanaotoa rushwa.

Walisema katika uchaguzi uliopita baadhi yao walishindwa kutokana na kutawaliwa na vitendo vya rushwa ambavyo wakati mwengine vilijitokeza wazi wazi.

Wakizunguma na mwandishi wa habari hizi kwa nyakati tofauti, walisema lazima ZAECA wajiandae kwa uchaguzi mkuu ujao.

Walisema ZAECA isisubiri kupelekewa malalamiko ya tuhuma za rushwa, bali itanue mbawa zake kama inavyofanya TAKUKURU kwa Tanzania Bara.

Aliekuwa mgombea wa ubunge jimbo la Ole kwa tiketi cha chama cha Umma, Maryam Saleh, alisema wapo baadhi ya wagombea wanaume mtaji wao ni rushwa ni mkubwa.

Alieleza kuwa, licha taasisi kadhaa ikiwemo Chama cha waandishi wa habari wanawake Tanzania (TAMWA- Zanzibar) ofisi ya Pemba kuwajengea uwezo na kuwa tayari kugombea, lakini bado rushwa ni donda ndugu.

Aliekuwa mgombea wa nafasi ya ubunge jimbo la Wawi, Mryam Mohamed Muhene kwa tiketi ya ADC, alisema kama rushwa haijadhibitiwa, wanawake wengi wataendelea kuyasikia redioni majimbo ya uchaguzi.

“Bado wapo wagombea wanaume, wanadhani majimbo yana hati miliki kwao, sasa ukiingia na ukionekana una dalili za kukubalika jimboni, rushwa hapo hutawala,’’alieleza.