NA ASYA HASSAN

CHAMA cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) Zanzibar, kimesema kilio cha wanawake kutaka kushika nafasi za juu za uongozi kimesikika baada ya kuapishwa kwa mama Samia Suluhu Hassan kuwa Rais wa sita wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Samia aliyekuwa Makamu wa Rais, aliapishwa kushika wadhifa huo Machi 19, 2021 baada ya kifo cha aliyekuwa Rais wa Tanzania marehemu Dk. John Pombe Magufuli, aliyefariki Machi 17, 2021 kutokana na ugonjwa wa moyo, jijini Dar es salam.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya dua maalum ya kuwaombea viongozi wa juu wa nchi wakiwemo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar Dk. Hussein Ali Mwinyi, Mkurugenzi Mtendaji wa chama hicho Dk. Mzuri Issa Ali, alisema hatua hiyo ni muhimu katika harakati za ukombozi wa wanawake.

Alisema hatua hiyo inadhihirisha kwamba wanawake wana uwezo wa kushika nafasi za uongozi na kuleta mabadiliko ya kiuchumi katika familia na jamii kwa ujumla.

“Kwa muda mrefu chama kimekuwa kikitoa elimu kwa jamii juu ya kuwachagua viongozi wanawake ili waweze kushika nafasi hizo kwa kuamini kwamba wana uwezo mkubwa wa kuitumikia jamii na kuleta mabadiliko mapana ya kimaendeleo ndani ya nchi yao,”alisema.

Alisema hiyo ni ishara tosha ya kuwaona kama wanawake wana uwezo wa kuwa viongozi na kuchochea ukuwaji wa uchumi wao. 

“Kupitia nafasi iliyokamatwa na kiongozi huyo, ni mfano wa uelewa mkubwa kwa wale waliokuwa wakipinga kwa namna moja au nyengine kama wanawake hawawezi kushika nafasi za uongozi,” alisema.

Kwa upande wa Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Mgeni Hassan Juma, alisema Rais Samia kwani atafanya vizuri katika kuyaendeleza yale mazuri yote yalioachwa na aliyemtangulia. 

Akizungumzia dua hiyo, alisema marehemu Rais Dk. John Pembe Magufuli, alikuwa akisisitiza kila kitu muhimu kumtegemea Mwenyezi Mungu ili kuzidi kuleta neema baraka na kuwafanya viongozi hao kuwatumikia wananchi kwa ufanisi na weledi. 

Akisoma risala baada ya kumaliza kusomwa kwa dua hiyo mwalimu Thania Mahmoud, aliwaombea viongozi hao kuweza kufanya kazi zao kwa ufanisi na kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria na kanuni za nchi. 

Thania ambae aliongoza kisomo cha dua hiyo, aliwatakia kheri wananchi pamoja na kuiombea dunia kukingwa na maradhi mbalimbali na majanga tofauti yanayotokezea. 

Dua hiyo imeandaliwa na jumuiya mbalimbali za wanawake ziliyopo hapa nchini pamoja na Umoja wa wanawake Tanzania (UWT) na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wanawake wakiwemo wake za mke wa Makamu wa Kwanza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.