NA MADINA ISSA

WAZIRI wa Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto, Nassor Ahmed Mazrui, amewataka wazazi wa kiume kuona umuhimu wa kushirikiana na wake zao kuwapeleka watoto wao katika vituo vya afya, ili kuweza kupatiwa chanjo

Waziri Mazurui, aliyasema hayo, wakati wa uzinduzi wa wiki ya chanjo Afrika, ambapo kwa Zanzibar uzinduzi huo ulifanyika kituo cha Afya cha Mwera, Mkoa wa Kusini Unguja.

Mazrui, alisema chanjo kwa watoto ni kinga muhimu kwa maradhi yanayozuilika na ni vyema kwa wazazi wa kiume kuwapa ushirikianao wake zao kufanikisha tiba hiyo, kwani baadhi wameonekana kutowaunga mkono.

Alisema chanjo ni muhimu kwa watoto katika kuimarisha makuzi yao na kuwafanya wawe na afya bora iwapo watapatiwa kwa ukamilifu na kwa wakati.

Aliwataka wananchi wasipuuze kuwapeleka watoto wao katika vituo vya afya kupatiwa chanjo, kwani kinga ni bora na rahisi kuliko tiba.

Alisema lengo la Afrika kuweka wiki maalumu ya chanjo ni kutoa fursa kwa watoto waliofika umri wa kupata tiba hiyo, kupelekwa katika vituo vya afya, ikiwa ni hatua itayowaondolea maradhi wakati wakiwa madogo.

Mkuu wa Mkoa Kusini Unguja, Hadid Rashid Hadid, alisema wananchi wa Mkoa huo wanamuamko mkubwa katika suala la chanjo na kwa mujibu wa takwimu wanaongoza kwa Mikoa yote ya Tanzania.

Hata hivyo, alimuhakikishia Waziri huyo, kwamba uongozi wa Mkoa huo utaendelea kusimamia na kufanya kila juhudi ili kuhakikisha watoto wote wanapatiwa chanjo kwani ni moja kati ya haki yao ya msingi.

Hata hivyo Mkuu huyo wa Mkoa alikiri kuwa wapo baadhi ya kinamama wachache ambao hawakamilishi chanjo kwa watoto wao na mkakati wa kuwahimiza utawekwa ili wakamilishe na kuendelea kuwa mfano kwa Mikoa mengine.

Kaimu Daktari zamana kituo cha Afya Mwera, Salma Bakari, alisema kituo hicho kimekuwa kikifanya vizuri katika kutoa chanjo za watoto ingawa bado kuna baadhi ya akinababa wamekosa mwamko na kuhisi kuwa kazi ya kuwapeleka watoto vituo cha afya ni kazi ya akinamama peke yao.

Kaulimbiu ya wiki ya chanjo Afrika mwaka huu ‘Chanjo huweka jamii pamoja.’