NA ASYA HASSAN
WANAWAKE wa Shehia ya Kibweni Wilaya ya Magharibi ‘A’Unguja, wamewaomba wananchi kuwainua na kuwawezesha wanawake wanaojitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi, ili waweze kushika nafasi hizo.
Walisema hatua hiyo itawapa moyo na ari wanawake kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali pale zinapotokezea.
Wanawake hao walisema hayo walipokuwa katika kikao cha pamoja kilichowashirikisha wananchi, wanaume wa mabadiliko pamoja na maofisa kutoka Chama cha waandishi wa habari Wanawake Tanzania (TAMWA,Zanzibar).
Walisema wapo baadhi ya wanawake wapo tayari kugombea nafasi za uongozi pale zinapotokezea, lakini wanashindwa kufanya hivyo kwa kuhofia kusemwa vibaya pamoja na kukosa mashirikiano ya kina kutoka kwa wananchi.
Sambamba na hayo walisema licha ya uwepo wa muamko mkubwa kwa wanawake wa visiwa hivi, lakini bado wanawake wengi hushindwa kufikia malengo yao kwa kile wanachokidai kukosa hamasa pamoja na kushindwa kuungwa mkono na watu wa karibu.
Kwa upande wa mwanaume wa mabadiliko Mohammed Jabir Makame, alisema jamii ya wanawake wanapaswa kubadili mitazamo yao na kuona kuwa wanawake wanaweza kuwa viongozi na sio kuwadharau na kuona kuwa hawawezi kufanya lolote lile.
Alisema licha ya kuwepo kwa harakati za kuwawezesha wanawake kushika nafasi hizo, lakini baadhi ya wanajamii wana uelewa mdogo unaowabainisha kwamba wanawake hawapaswi kuwa viongozi.
“Changamoto ni mifumo iliyopo bado inawasababisha wasiende kugombea nafasi hizo pamoja na kukosa mashirikiano ya kina kwa jamii pale mwanamke anapokuwa tayari kugombea,”alisema.
Kwa upande wa sheha wa shehia ya Kibweni Subira Haji Yahya alisema endapo wanawake wakipatiwa nafasi ya kuongozo wanauwezo mkubwa wa kuleta mabadiliko makubwa katika nyanja mbalimbali ikiwemo uchumi, kijamii na maeneo mengine.
“Wanawake wanauwezo mkubwa wa kuleta mabadiliko katika maendeleo lakini kinachowarudisha nyuma ni mfumo dume uliyotawala katika nyoyo za binadamu ndio unaochangia kurudisha nyuma harakati za kuwainua wanawake katika kushika nafasi hizo,”alisema.
Ofisa Miradi kutoka TAMWA Zanzibar, Sabrina Yussuf Mwitanga, alisema taasisi hiyo itaendelea kuielimisha jamii hususan dhana ya uongozi kwa ili waweze kuwaunga mkono na kuongeza idadi ya viongozi wanawake kupitia nafasi mbalimbali.
Awali TAMWA ilifanya kikao kama hicho katika shehia ya Donge Karange Wilaya ya Kaskazini ‘B’ Unguja na kuwahamasisha wananchi wa maeneo hayo kutoa fursa zaidi na kuwaunga mkono wanawake kugombea nafasi hizo.
Tamwa-Zanzibar inasimamia mradi wa kuwainua wanawake wa Zanzibar waweze kushiriki katika vyombo vya kutoa maamuzi, mradi ambao unafadhiliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa lililojihusisha na haki za wanawake (UN WOMEN).