NAIROBI, KENYA
ZAIDI ya paketi 24,000 za dawa za kupunguza makali ya virusi vya UKIMWI zilizosambazwa katika majimbo 31 nchini Kenya zina athari kubwa kwa wale wanaozitumia.
Wanaharakati wa maswali ya HIV wanasema matumizi ya dawa hizo zenye thamani ya shilingi za Kenya bilioni 1.2 yalisitishwa nchini humo mnamo mwaka 2019.
“Kwa nini serikali inacheza na maisha ya watu? Tumewaambia mara nyingi sana kwamba dawa hizi hazifanyi kazi kwa sababu madhara ambayo yamehusishwa nayo”, alisema Nelson Otuoma.
Dawa iliyosimamishwa ni ile ya zidovudine / lamivudine / nevirapine, ambazo ni ni miongoni mwa dawa zilizotolewa kama msaada kwa nchi kutoka mfuko wa ule Global Fund na mpango wa dharura wa rais wa Marekani wa Usaidizi wa Virusi vya HIV (PEPFAR).
“Tumeshangazwa sana kwamba dawa hizi zilikuwa bado kwenye ghala kwa miezi na walituambia kuwa zilikuwa zimeshaharibiwa”, alisema Otuoma.
Kwa kawaida, dawa ya nevirapine, hutolewa kama dawa moja au kama mchanganyiko wa kipimo cha dawa tatu.
Madhara ya dawa hii kwa kawaida ni maumivu ya tumbo, upele, uchovu, maumivu ya kichwa, kutapika na maumivu ya misuli, ambayo huenda baada ya mwezi mmoja.
Nevirapine imehusishwa pia na uharibifu wa ini kwa watumiaji ambapo nchi nyingi zimesitisha matumizi yake kwa watu wanaishi na HIV.
Shirika la Afya Duniani (WHO) limesema kwamba matibabu ya msingi wa Nevirapine yalikuwa yameonesha kiwango kikubwa cha kutopunguza makali ya virusi vya ukimwi mwilini.