WAUMINI wa dini ya kiislamu visiwani Zanzibar wanaungana na waislamu wenzao wote duniani kuianza ibara ya swaum ambayo ni nguzo ya nne katika uislam.

Ibada hii wamefaradhishwa kwa waislamu na wametakiwa waitekeleze ambapo katika mwaka hutekelezwa ndani ya mwezi maalum na huwa kati ya siku 29 ama 30 za mwezi huo.

Zipo faida nyingi za kufunga zinazojulikana na kuonekana wazi na zile zisizoonekana, ikiwemo malipo makubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa wale waliofunga kwa nia safi na kwa ajili yake.

Tungependa kuwatahadharisha sana waislamu kuwa kuna tofauti kubwa sana baina ya kufunga na kujizuia kula, kufunga kuna masharti yake na lazima yatimie ili mja aweze kupata fadhila za ibada hiyo.

Kwa mfano mwenye kufunga lazima aazimie kuweka nia mahususi ya kufanya ibada hiyo kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na si vyenginevyo, pia kuacha kutekeleza yale yote yanayobatilisha funga.

Si jukumu letu kuhukumu, lakini mtu ambaye atafunga kwa ajili tu watu wamefunga na pengine anaona haya kula kwa sababu watu wamefunga na  hakuweka nia hatudhani kama anaweza kupata malipo yaliyoahidiwa.

Aidha mtu aliyefunga lakini akiwa hana tofauti kwenye kauli na vitendo vyake baina ya mwezi wa swaumu na miezi mingine, bila shaka swaumu zake zitakuwa na hitilafu kubwa.

Mtu aliyefunga hubadilika kitabia na ibada hiyo humgeuza kuwa mtu mwema, kama alikuwa na vitendo viovu na vichafu kama vile wizi, uzinzi, usengenyaji, ulevi, ghilba, kuchonganisha watu na mengineyo yaliyokatazwa mambo hayo si wakati wake katika mwezi huu.

Watafiti wengi wa matibabu ya mwanadamu wameifanyia utafiti swaum na kubaini kuwa ni jambo lenye faida kubwa kwa uimarishaji wa afya.

Zipo hospitali mbalimbali zinazohimiza na kusisitiza umuhimu wa kupunguza ulaji ovyo, ambao ndio chanzo cha maradhi kadhaa mwilini ikiwemo mtu kuwa na uzito mkubwa.

Katika utafiti alioufanya Daktari wa Chuo kikuu cha Cairo, Muhammad Dhawahir, alisema ‘Ugonjwa wa kuzidi maji mwilini, unene, moyo, ini, pafu na mengineyo huzuiwa kwa mtu kufunga swaumu’.

Kuna kila sababu ya waislamu kuitekeleza nguzo hiyo muhimu ya dini, kwanza kwa kutaraji malipo makubwa yaliyoahidiwa na yule aliyeifaradhisha ibada hiyo.

Aidha umuhimu mwengine kwa waislamu katika kutekeleza ibada hii ni kuziimarisha afya zao na kuepukana na maradhi sugu ambayo yamekuwa yakizikabili jamii zetu.

Kwa upande wa Zanzibar ni vyema wakati huu wa ibada ya swaum watu tukafanyiana wema, kuzidisha huruma, kuzidisha upole na kuongeza mapenzi huku tukimtanguliza Mwenyezi Mungu.

Haipendezi kwa wafanyabishara kutumia msimu huu kuwakomoa wananchi kwa sababu wanahitaji chakula cha futari ndio wakakomolewa kwa kuuziwa kwa bei ya juu.

Wafanyabishara lazima wakumbuke kuwa faida watakayoipata kwa kuuza bidhaa kwa bei ya juu thamani yake ni ndogo sana, kwa sababu faida hiyo huishia kwenye maisha ya duniani.

Ni jukumu la wafanyabishara vile vile kuepuka hadaa kwenye bidhaa wanaoziuza, kwani huu ni wakati wa kuuziwa polo la chenga za makaa, muhogo mchungu huku muuzaji akiapa kwa jila la Mungu kuwa muhogo wake mtamu na unawiva.

Ni vyema sana waumini wa kiislamu wakaitekeleza ibada hii kwa kumtangulia Mwenyezi Mungu, sambamba na kufuata kwa masharti ya ibada yenyewe.