NA MWANDISHI WETU

WAZIRI wa TAMISEMI,  Ummy  Mwalimu, amemsimamisha kazi Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema,  Magesa Boniphace kupisha uchunguzi.

Taarifa iliyotolewa na kitengo cha Mawasiliano Serikalini imeeleza kuwa, Waziri Ummy amechukua hatua hiyo baada ya kupokea malalamiko na tuhuma za ubadhirifu wa fedha za miradi ya maendeleo katika halmashauri hiyo kutoka kwa wananchi na viongozi mbalimbali akiwemo Mbunge wa Sengerema (CCM), Hamisi Tabasamu.

Taarifa hiyo, imefahamisha kuwa tuhuma hizo zimeelekezwa kwa Mkurugenzi na baadhi ya wakuu wa Idara za Halmashauri hiyo.

Taarifa hiyo imeeleza kwamba watendaji hao wanafanya ubadhirifu na matumizi mabaya ya fedha za umma zilizotengwa kwa ajili ya shughuli za maendeleo katika halmashauri hiyo, na kuathiri utekelezaji wa miradi kwa kiwango kilichokusudiwa.

Kufuatia tuhuma hizo, Ummy amemuagiza Katibu Mkuu TAMISEMI kuunda timu ya uchunguzi wa tuhuma hizo haraka.

Pia, amemuelekeza Mkuu wa Mkoa wa Mwanza kuhakikisha katika kipindi chote ambacho timu ya uchunguzi itakua ikifanya kazi katika halmashauri hiyo, malipo yote yatakayofanyika kuanzia sasa yazingatie sheria, kanuni na taratibu za usimamizi wa fedha za umma.