NA MWANDISHI WETU, DODOMA
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa TAMISEMI, Ummy Mwalimu, ameagiza watendaji wote waliotajwa katika ripoti ya mkaguzi na mdhibiti wa hesabu za serikali CAG, kuchukuliwa hatua za kisheria.
Waziri Ummy, ametoa wito huo jijini Dodoma wakati akizungumza viongozi na watumishi wa ngazi zote katika Mkoa wa Dodoma.
Waziri huyo alikutana na viongozi hao kwa dhamira ya kuweka mikakati ya pamoja katika kuendesha Wizara hiyo, ambapo alisema sekretarieti za Mikoa ndizo zenye wajibu wa kumshauri Mkuu wa Mkoa juu ya masuala mbali mbali yanayohusu Mkoa husika.
Alisema watakao bainika wote waliohusika katika ubadhilifu, waliosababisha au uzembe uliofanywa hadi kupelekea halmashauri kupata hati chafu au hati yenye mashaka lazima wachukuliwe hatua stahiki.
Kutokana na hatua hizo amezitaka sekretarieti za Mikoa yote hapa nchini kuhakikisha zinatimiza wajibu wake kwa weledi na kuongeza kasi katika kushauri masuala mbalimbali yanayohusu maendeleo ya Mikoa hiyo hasa katika ukusanyaji wa mapato ya serikali.
Vile Vile, Waziri Ummy amewataka viongozi hao kujenga utaratibu wa kuzitembelea halmashauri zote za Mikoa, na kwenda kufanya tathmini ya mipango na utekelezaji wake kwa kila robo ya mwaka, ili kubaini vikwazo na kuzitatua kwa wakati, ili kufikia malengo waliyojiwekea katika halmashauri husika.
“Kila robo ya mwaka mkae kwa pamoja aidha muwaite kwenu au muende kwao mkakae kwa pamoja muangalie mipango yenu imefikia wapi, walitakiwa wakusanye kiasi flani kwanini hawajafika lengo, kuna fedha imekusanywa kwanini haijaingizwa benki, kuna mradi hawajaomba fedha kwanini” amesema Waziri Ummy.
Waziri huyo amewataka kuongeza kasi ya utatuzi wa kero za wananchi, kwani kuna malalamiko mengi sana katika maeneo mbalimbali hasa katika masuala ya ardhi na lazima wajenge tabia ya kuwasikiliza wananchi kero zao, na sio kuwa wao ndio wawe wazungumzaji pekee.
“Nilikuwa nazungumza na wakuu wa Mikoa wa zamani wanasema wao walikuwa wakienda hadi ngazi za chini kabisa, lakini sasa hivi huo utaratibu umepungua, nataka wakuu wa Mikoa muende hadi ngazi za kata mkae huko msikilize kero za wananchi na wakuu wa Wilaya waende hadi ngazi za Kijiji” amesema.
Amepongeza juhudi kubwa zilizofanyika katika Mkoa wa Dodoma katika utendaji kazi na utekelezaji wa miradi na kuwataka kuongeza kasi.
Waziri huyo amepongeza katika sekta ya elimu kwa kuongeza ufaulu kwa skuli za msingi kutoka ufaulu wa asilimia 53 hadi kufikia asilimia 76 na sekondari kutoka asilimia 64 hadi kufikia asilimia 87.
Amepongeza juhudi zilizofanyika hasa katika miradi ya elimu katika ujenzi wa vyumba vya madarasa, matundu ya vyoo na ujenzi wa maabara kwa skuli za sekondari, sambamba kwenye sekta ya afya na miondombinu yake.