NA KHAMISUU ABDALLAH

WAZIRI wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Simai Mohammed Said, amesema matumizi ya teknolojia yana mchango mkubwa katika kuinua ubora wa elimu na suluhisho la changamoto zinazoikabili sekta hiyo.

Kauli hiyo aliitoa wakati akifunga mkutano wa siku tatu wa kutathmini maendeleo ya elimu ya sekta elimu Zanzibar uliofanyika katika hoteli ya Madinat Bahr.

Alisema, sekta hiyo ina changamoto nyingi ambazo zinaathiri ubora wa elimu inayotolewa ikiwemo za uhaba wa walimu wa sayansi, uhaba wa vifaa vya kujifunzia na kufundishia (vitabu).

Waziri Simai alibainisha kwamba changamoto hizo zinaweza kutatuliwa kwa matumizi sahihi ya teknolojia kwa wanafunzi katika skuli zote za Unguja na Pemba.

Hata hivyo, alibainisha kuwa teknolojia inaweza kuwa njia mbadala ya kuendelea kuwasomesha wanafunzi popote walipo hasa wakati wa majanga.

Alisema matumizi ya teknolojia ni chachu ya kufikia malengo yaliyowekwa na serikali katika dira ya maendeleo ya Zanzibar 2050 na malengo ya maendeleo endelevu (SDGs) ifikapo mwaka 2030.

Hivyo alibainisha kuwa maazimio waliyofikia katika mkutano huo yataisaidia wizara kujipanga vizuri katika kuharakisha matumizi ya teknolojia katika ngazi zote za elimu kuanzia maandalizi, msingi, sekondari, elimu ya juu, vyuo vya mafunzo ya amali, vyuo vya ualimu na vyuo vikuu.

Sambamba na hayo, alisema hayo yote yatafanikiwa ikiwa wadau wote watajikubalisha kufanya kazi kwa bidii na hamu ya kuiletea nchi maendeleo ya haraka.

Mwenyekiti wa Kamati ya Ustawi wa Jamii Baraza la Wawakilishi, Yahya Rashid, aliwaomba wadau mbalimbali walioshiriki katika tathmini hiyo kushirikiana na kujenga mshikamano wa pamoja katika kuona changamoto zote zinazoikabili sekta hiyo zinafanyiwa kazi inavyotakiwa.

Hata hivyo, alibainisha kuwa, mashirikiano ya dhati na uwajibikaji katika sekta zao ndio nguzo muhimu kuona suala la teknolojia katika kuendeleza elimu Zanzibar wanapiga hatua ambayo wanaitarajia katika sekta hiyo.

“Kazi hii itakuwa rahisi ikiwa tutashirikiana pamoja katika sekta binafsi na serikali katika kujenga umoja wetu katika kuinua kiwango cha elimu nchini kwetu,” alibainisha.

Nae, Mwakilishi wa mtandao wa elimu kwa wote Zanzibar Ali Bakar Hamad, aliipongeza serikali kwa kuweka mazingira mazuri ya upatikanaji wa elimu hasa kwa watu wenye ulemavu hasa kutayarishwa katika kutumia teknolojia katika ngazi ya vyuo vikuu na katika maskuli.

Hivyo, walitoa mapendekezo kwa serikali ikiwemo kutilia mkazo suala la teknolojia na kubadilika kisera kiutendaji na mfumo mzima wa ufatiliaji.

Hata hivyo alisema mikakati ya elimu kuipitia upya ili kuweka mipango mizuri inayokwenda sambamba na mahitaji ya sasa kwa wanafunzi kwani mazingira ya sasa yanahitaji ubunifu katika ngazi mbalimbali ikiwemo katika ufatiliaji.

Mbali na hayo, alisema imefika wakati kwa sasa kupata sera ya elimu ambayo itatoa matamko ya wazi na yapamoja ya muelekeo wa sayansi na teknolojia na sera hiyo ieleze wazi juu ya majukumu ya vyuo vikuu katika kusaidia muelekeo wa elimu Zanzibar.

Hata hivyo, alibainisha kwamba kuona fursa zilizokuwepo katika teknolojia na kuziwekea mikakati madhubuti ili kutoachwa nyuma kitaifa kimataifa na kikanda.