NA MWAJUMA JUMA

WIZARA ya Elimu na Mafunzo ya Amali, imeombwa kuwaangalia na kuwaandalia mazingira bora   waalimu wanaofundisha madarasa kuanzia maandalizi hadi darasa la sita, ili kuwepo katika hali ya usalama.

Ombi hilo, limetolewa na wanafunzi wanaosomea ualimu katika Chuo cha Kiislamu Zanzibar, wakati wa Mafunzo ya Afya na Usalama Kazini, yaliyotolewa na Idara ya Afya na Usalama, kazini huko Mazizini Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.

Mwalimu Menuu Abdalla Mbarouk, alisema wanakubali kwamba hiyo ni moja ya  kazi yao,  lakini ni vyema kwa Serikali kuwaangalia wa kina waalimu hao ambao wanakuwa na Kazi kubwa katika ufindishaji wao.

Alisema waalimu wanaosomesha madarasa hayo wanakuwa na kazi kubwa katika ufundishaji tofauti na wale ambao wanasomesha madarasa ya juu.

“Tunaikubali kazi yetu sawa lakini lazima na sisi tuangaliwe sana katika suala la ufindishaji hasa wa madarasa ya chini mpaka darasa la sita”, alisema.

Alisema kuna baadhi ya waalimu wakuu wanatumia vibaya wadhifa wao kwa kuwapangia vipindi waalimu bila kuwashirikisha sambamba na kuwapangia masomo ambayo sio waliyosomea.

Nae Mwalimu Farashuu Khamis Ramadhan, alifahamisha matatizo yote ambayo huwapata waalimu yanaweza kutatulika kwa vitu endapo Serikali itaongeza majengo, vitendea kazi, na wafanyakazi na suala hilo si kwa waalimu bali ni kwa taasisi zote ili wafanyakazi wawepo katika hali ya usalama.

Kwa upande wake mwanafunzi Omar Mohammed, amesema ipo haja kwa waalimu kupatiwa muda maalumu na wa mara kwa mara wa kuchunguzwa Afya zao ili kuwajua .

Alisema walimu kutokana na mazingira yao ya ufundishaji hawapo salama kiafya, hivyo kufanyiwa uchunguzi wa kiafya mara kwa mara kutawasaidia kujua mapema athari ambazo wanaweza kuzipata.

“Mwalimu mmoja kwa siku anakuwa na vipindi zaidi ya vitatu na wanafunzi kwa darasa moja hawapunguwi 60 sasa inafika wakati mwalimu mmoja anatakiwa kusainisha mabuku zaidi ya 180 jambo ambalo ni hatari wa Afya yake hasa kwa vile ni kitendo cha kila siku”, alisema.

Hivyo kama Serikali itaongeza majengo na kuwaajiri waalimu wengi kwa kiasi wanaweza kuondokana na changamoto hiyo.

Afisa Msajili na Mkaguzi kutoka Idara ya Usalama na Afya Kazini Ame Faki Saleh amewataka waalimu hao kujitahidi kutenga muda wa mapumziko ili kujiweka katika hali ya usalama.

Alifahamisha kwamba wanajua kazi ya ualimu ni ngumu na ina vipindi vingi vya kufundisha, ingawa kuajiri ndie anajukumu la kuhakikisha afya na usalama kwa wafanyakazi wake, lakini lazima na wao wajipangilie ili kujiepusha kujiumiza.