NAIROBI, KENYA

NAIBU rais wa Kenya William Ruto ametishia kukihama chama cha Jubilee iwapo kitaendelea kuwavuruga viongozi wanaomuunga mkono, huku akisema yuko tayari kukitumia chama kipya UDA kugombea urais kwenye uchaguzi mkuu ujao.

Katika mahojiano na kituo kimoja cha televisheni nchini Kenya, Ruto alionekana akiwa na jazba, alisikitishwa na jinsi wabunge wanaomuunga mkono walivyotimuliwa kwenye nafasi za uwenyeviti wa kamati za bunge.

Katika mahojiano hayo Ruto alisema baadhi ya mawaziri wanaomuunga mkono wametimuliwa kwenye nafasi zao huku wakibambikizwa mashitaka ya kuhusika na ufisadi.

Miongoni mwa wanasiasa wanao muungamkono Ruto walioondolewa katika nafasi zao ni pamoja na seneta wa Elgeyo-Marakwet, Kipchumba Murkomen, ambaye aliondolewa kwenye nafasi ya kiongozi wa wengi katika bunge la seneti.

“Ningali na matumaini kwamba chama cha Jubilee kitabadilika na kurejea kwenye maono ya awali, lakini hilo lisipofanyika, lazima tuwe na mikakati, sisi tuna bahati kwa sababu tuna chama cha UDA

Naibu rais huyo alisema bado ana matumaini makubwa na rais Uhuru Kenyatta, lakini chama cha Jubilee kikiendelea kuvuruga mambo atafirikia kuondoka na kujiunga na chama cha UDA ambapo atasimama kuwani urais.

Mahusiano kati Ruto na Uhuru Kenyatta yanaonekana kuingia doa baada ya Ruto kusema atagombea kiti cha urais, kwenye uchaguzi mkuu ujao, ikiwa Kenyatta atamuunga ama asipomuunga mkono.