NA RAYA HAMAD,   OMKR                                

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais,  Dk Saada Mkuya Salum,   amesema Ofisi yake itasimamia vyema majukumu yake, ili kuhakikisha masuala yote mtambuka yanakuwa salama na hayaathiriwi 

Akitoa taarifa ya  utekelezaji wa programu za ofisi yake kwa kipindi cha miezi mitatu Januari na Machi 2021, aliyoiwasilisha kwa Kamati ya inayosimamia Ofisi za viongozi wakuu wa Kitaifa ya Baraza la Wawakilishi.

Dk. Saada amesema, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais moja kati ya malengo yake ni kuhakikisha inakuwa na mfumo bora wa kisera na kisheria kwa taasisi inazozisimamia

Aidha, amesema Kupitwa na muda kwa baadhi ya Sera na Sheria zinazosimamiwa na Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, ni changamoto ambayo tayari imeanza kufanyiwa kazi, kufanyiwa mapitio na kutoa  mapendekezo ya kurekebisha Sera na Sheria hizo  kwa ajili ya utekelezaji, ili kuendana na kasi ya kiutendaji kwa mujibu wa taratibu

‘Rasimu ya Sera ya Dawa za Kulevya imeandaliwa na ipo katika hatua ya kuwasilishwa Baraza la Mapinduzi. Rasimu ya Sera ya Mazingira ipo katika hatua ya maandalizi na rasimu ya marekebisho ya Sheria ya Watu Wenye Ulemavu, ipo katika hatua ya kupelekwa kwa wadau’alifafanua Dk. Saada

Nae Mwenyekiti wa Kamati ya inayosimamia Ofisi za viongozi wakuu wa Kitaifa ya Baraza la Wawakilishi,  Hassan Khamis Hafidh, ameiomba Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais kuhakikisha wanasimamia vyema majukumu yao, ili Zanzibar iendelee kuwa salama kwa masuala wanayoyaratibu.

Hassan, amesema Zanzibar inahitaji kuwa salama katika kulinda na kuhifadhi mazingira, kutokubali kuwa ni sehemu ya wapitishaji na wauzaji na wasambazaji dawa za kulevya, kuzingatia vyema masuala ya upatikanaji wa haki za  Watu wenye Ulemavu na kuwa na jamii isiyokuwa na maambukizi ya virusi vya Ukimwi na UKIMWI

Aidha, amewataka viongozi wa Ofisi hio kuhakikisha matumizi na mapato yanaendana na utekelezaji wa mpango wa bajeti,

Mkuu Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Khadija Khamis Rajab, alisema  mradi wa kujenga uwezo wa kuhimili na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi  kwa maeneo ya pwani  katika eneo  la Kilimani, amesema mafaniko makubwa yamepatikana katika mradi huo.

Alisema hifadhi ya fukwe imerudi ukilinganisha awali maji yalikuwa yakiingia karibu na maeneo ya makaazi.

 Mradi huo ambao umefadhiliwa na Mfuko wa Dunia wa kimazingira ulianza 2013/ 2018 na shughuli zilizofanyika katika kurudisha mazingira  ni upandaji wa mikoko ,na kuweka ukuta kwa kutumia  mawe kwa ajili ya kuzuia maji ya bahari yasipande juu.

Hatua hiyo imechukuliwa ili kuzuiya kuathiri maeneo ya makaazi ambapo shughuli hizo zimegharimu zaidi ya dola za kimarekani 400,000 zilizosimamiwa na wahisani wenyewe

Aidha, katika kuliendeleza eneo mradi ulipewa Jumuiya ya kuhifadhi na kusimamia  mazingira ZACEDY na hatua kadhaa zilichukuliwa ikiwemo kutoa elimu kwa jamii, viongozi wa Wilaya na Shehia, ili wapate uelewa,  usafishaji wa eneo,  masuala ya ufatiliaji na tathmini, shughuli za upandaji miti ambapo gharama zilizotumika ni zaidi ya Milioni 11.

Katibu wa Jumuiya inayosimamia mazingira  ZACEDY kwa maeneo ya pwani  ya Kilimani, Jamal Khamis Juma, amesema kwa kiasi kikubwa wamefanikiwa kurudisha eneo hilo kwa kushirikiana na Ofisi ya Wilaya Mjini na wanajamii.

Pia  ametoa shukurani kwa  Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupitia Idara ya Mazingira na Mamlaka ya usimamizi wa Mazingira kwa kuaminiwa na kuliendeleza eneo hilo  .