WAPENDA haki na usawa duniani kwa hakika na wanaushahidi kwamba ulimwengu hauendeshwi kwa usawa na ndio maana ulimwengu unakabiliwa na changamoto nyingi katika maeneo mbalimbali.

Mifumo ya ubebari inayong’ang’aniwa na mataifa ya magharibi imendelea kuwa kandamizi na inalindwa kwa nguvu na gharama zote na mataifa ya magharibi kwa sababu inafaida kubwa kwa upande wao.

Viongozi mbalimbali duniani wamekuwa wakielezea juu ya dunia kuwa na mifumo ya usawa, lakini kwa bahati mbaya sana pale unapoanza kufunua mdomo ndio unaanzisha vita na mataifa ya magharibi.

Hata hivyo, bado wapo viongozi majasiri wanapopata fursa kwenye majukwaa makubwa huwa hawasiti kuendelea kuuelezea ulimwengu kuwa hauko katika hali ya usawa.

Kionngozi wa karibuni kabisa kueleza kufunua mdomo kwa ujasiri kuelezea kuwa ulimwengu hauko katika misingi ya usawa ni rais wa China, Xi Jinping ambaye amebainisha kuwa mfumo wa utawala wa kilimwengu lazima ufanywe uwe wa usawa na uadilifu zaidi.

Akizungumza kwenye Jukwaa la Boao, ambalo ni mbadala na Jukwaa la Kiuchumi la Davos na lililo maalum kwa mataifa ya Asia, rais huyo wa taifa la pili kwa nguvu ulimwenguni alisema dunia inahitaji zaidi haki na sio utawala wa kundi ama nchi moja.

Xi Jinping alifikisha ujumbe huo pahali panapostahiki hasa ikizingatiwa mkutano huo ulihudhuriwa na viongozi kadhaa wakiwemo Rais Joko Widodo wa Indonesia, rais Thongloun Sisoulith wa Laos, rais Jae-in Moon wa Korea Kusini, rais Halimah Yacob wa Singapore na rais wa Shirika la Fedha Duniani (IMF), Kristalina Ivanova Georgieva-Kinova.

Rais Xi Jinping alisema kwamba kanuni zinazowekwa na nchi moja ama baadhi ya mataifa zisilazimishwe kufuatwa na mataifa mengine, alisema hayo bila ya kuzitja nchi zenye tabia ya kupitisha sera na kulazimisha zifuatwe na nchi nyengine.

Xi Jinping aliwaambia washiriki wa jukwaa hilo kwamba kujenga vizuizi na kulazimisha mgawanyiko kutawaumiza watu wote na kamwe hakufaidishi hata mmoja.

Akitoa hotuba hiyo iliyokuwa ikisubiriwa kwa hamu na kwenye ukumbi uliokuwa na utulivu, rais Xi alisema kuwa dunia ya sasa inapaswa kukataa kurejea kwenye zama za vita baridi, huku akisema China itaendelea kupunguza orodha aliyoiita ‘hasi’ kwa ajili ya uwekezaji wa kigeni.

Kwa muda mrefu sasa, China imekuwa ikitaka kuweka mageuzi makubwa kwenye namna ulimwengu unavyosimamiwa, ikipigania mitazamo na maadili ya nchi nyingi nyengine kuakisika, yakiwemo ya China yenyewe, na sio mataifa machache yenye nguvu duniani.

Mara kadhaa, Beijing imepambana na wadau wakubwa wa usimamizi wa ulimwengu, hasa Marekani, juu ya masuala kadhaa kuanzia ya haki za binaadamu hadi ushawishi wa kiuchumi wa China kwa mataifa mengine.

“Nchi kubwa ionekana kubwa kwa kuonesha kubeba wajibu mkubwa zaidi, lakini ukubwa huo usiwe kigezo cha kuwalazimisha wengine waifuate vile nchi kubwa inavyotaka”, alisema rais Xi.

Katika mkutano huo, rais Xi Jinping aliwaeleza viongozi hao kuwa taifa lake litaendelea na sera yake ya kushirikiana na mataifa mbalimbali katika mipango yake.

Alisema China inaelewa matatizo yanayozikabiliwa nchi mbalimbali, hivyo itakuwa tayari kusaidia kwenye miradi ya afya katika kuzuia magonjwa, kuongeza ustawi wa afya ya jamii pamoja na matumizi ya dawa za asili.

Aidha alifahamisha kuwa Beijing itaendelea kushirikiana na wadau hasa katika ujenzi wa miundombinu kwa kile inachoamini kuwa ujenzi wa miundombinu ndiyo inayoharakisha maendeleo katika mataifa mbalimbali.

Hata hivyo taifa hilo la pili kwa nguvu za kiuchumi duniani limeendelea kutengwa na mataifa ya magharibi ikiwemo Marekani.

Itakumbukwa kuwa hivi karibuni rais Joe Biden wa Marekani aliitisha mkutano wa kwanza wa kilele wa ana kwa ana na waziri mkuu wa Japan Yoshine Suga, ambapo China ilikuwa kwenye ajenda ya mwanzo kabisa.

Mkutano Biden na Yoshihide Suga ulifanyika ikiwa njia moja wapo ya kurejesha ushawishi wa Marekani ulioporomoka, huku China ikiendelea kuyafikia maeneo mbalimbali duniani kutokana na kuwa na sera nzuri za mashirikiano na mahusiano.

Kama ishara ya wazi wa ushirikiano wa kiuchumi baina ya Marekani na Japan na katika kuitenga China, Biden alisema Marekani na Japan zitawekeza kwa pamoja kwenye miradi kama vile teknolojia ya mawasiliano ya 5G, maarifa ya kompyuta na biashara ya mitandaoni.

Hivi sasa taifa hilo limepiga hatua kubwa baada ya kufanikisha mikakati ya kutomeza umasikini kwa wananchi wake wanaofikiwa milioni 100 wanaoishi kwenye maeneo mbalimbali hasa vijijini.

Mataifa ya Afrika ambayo yana wananchi wengi masikini wanaweza kuiga mikakati iliyochukuliwa na China ambayo imefaikisha kutokomeza umasikini na kuinia hadhi za maisha ya wananchi wao.