NA TIMA SALEHE, DAR E SALAAM
KIKOSI cha Yanga SC, kinatarajia kuanza mzunguruko wake walala salama kwa kuvaana na KMC.
Mchezo huo utachezwa Aprili 10 kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam.Mchezo uliopita dhidi ya KMC Yanga waliibuka na ushindi wa mabao 2-1, kwenye Uwanja huo.
Mabao ya Yanga yalifungwa na Tuisila Kisinda, Waziri Junior huku bao la KMC likiingizwa kimiani na Hassan Kabunda.
Yanga itaingia dimbani ikiwa na kocha Juma Mwambusi baada ya aliyekuwa kocha wake mkuu Cedric Kaze kutimuliwa sambamba na benchi lake la ufundi kutokana na timu kutokuwa na mwenendo mzuri.
Akizungumza na Zanzibar Leo, mshambuliaji wa timu ya Yanga, Waziri Junior alisema ligi ilisimama kwa muda mrefu na wamefanya maandalizi ya kutosha hivyo wanaimani watafanya vizuri.
Alisema kama atapata nafasi atapambana kwa uwezo wake wote ili kuwapa raha mashabiki wao, lakini pia kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kutwaa ubingwa.
“Tunapambana kuhakikisha tunapata ushindi kwenye kila mchezo ili tujiweke kwenye nafasi nzuri,” alisema.
Yanga wanashika nafasi ya kwanza kwenye msimamo wa ligi hiyo wakiwa na pointi 50 wamecheza michezo 23 wameshinda 14 na kupoteza mmoja huku wakitoa sare michezo minane.