NA HAFSA GOLO

SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar, imesema inatumia gharama kubwa katika kuhakikisha wananchi wa maeneo mbali mbali wanapata huduma ya maji safi na salama ili kuondokana na kadhia ndani ya mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mjia Zanzibar (ZAWA),Mussa Ramadhan Haji, alieleza hayo jana wakati akizungumza na gazeti hili ofisini kwake Mabluu.

Alisema katika kuhakikisha hatua hiyo, inafikiwa kwa siku ZAWA inasambaza lita za maji elfu 50 ,000 na  inatumika lita 200 za mafuta.

Aidha Mussa alisema,utekelezaji wa zoezi hilo serikali kupitia ZAWA inahakikisha wananchi wote  wanapata huduma ya maji safi na salama katika kipindi hichi cha mwezi mtukufu wa Ramadhan, ili kuondosha usumbufu.

Alisema utoaji wa huduma hiyo unazingatia zaidi maslahi ya wananchi bila ya ubaguzi wa aina yoyote.

“Hii ni sadala ya serikali  na itahakikisha watu wote wanapata huduma hii mjini na vijijini ikiwa  ni agizo la Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Hussein Mwinyi”,alisema.

Hivyo Mkurugenzi huyo aliwasihi Masheha wa shehia kufatilia kwa karibu upatikanaji wa huduma hiyo na pale itapobainika ipo changamoto wasisite kutoa taarifa Zawa ili hatua stahiki zichukuliwa.

Pamoja na hayo aliwasihi wananchi kutumia vyema huduma hiyo  na waepuke kufanya israfu hasa ikizingatiwa serikali inatumia kiwango kibwa cha fedha.

“Hivi sasa ni mapema kueleza kiwango cha fedha kinachotumika kwani mahitaji kwa  kila siku yanaendelea kuibuka katika maeneo mbali mbali nchini “,alisema.