NA MWAJUMA JUMA

SHIRIKISHO la Soka Zanzibar (ZFF) limetangaza majina ya benchi la ufundi la timu ya Taifa ya Zanzibar ‘Zanzibar Heroes’ itakayoshiriki michuano ya nchi zisizokuwa wanachama wa FIFA (CONIFA).

Benchi hilo linaongozwa na kocha mkuu Hababuu Ali alitangazwa wiki mbili zilizopita, litakuwa chini ya meneja Hashim Salum.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi Kaimu Katibu wa shirikisho hilo Kibabu Haji Hassan, alisema katika benchi hilo wameongeza kocha msaidizi mwengine ili kuongeza nguvu zaidi.

Alieongezwa kushika nafasi hiyo ni Abdul Mutrik ‘Kiduu’ ambae atashirikiana na kocha Sheha Khamis katika kazi ya usaidizi.

Wengine walioitwa katika benchi hilo la ufundi ni Haji Makame Haji daktari mkuu na Mohammed Said anakuwa msaidizi wake wakati mtunza vifaa ni Abdulrahman Mohammed.

Awali shirikisho hilo lilitangaza kocha mkuu wa timu hiyo, msaidizi wake Sheha Khamis na kocha wa makipa Mohammed Abass, ambapo baada ya kuongezwa watu hao italifanya benchi hilo kuwa na watu saba.

Michuano ya CONIFA ambayo yanashirikisha nchi zisizokuwa wanachama wa FIFA yanatarajiwa kufanyika visiwani Zanzibar ambapo awali yalipangwa kufanyika mwezi ujao lakini kutokana na kuingia kwa mwezi mtukufu wa Ramadhan huenda yakasogezwa mbele.