NA MARYAM HASSAN

MFUKO wa Hifadhi ya Jamii (ZSSF) umewasilisha mpango kazi  kwa wadau wake unaolenga kuongeza mafanikio kwa wadau huo na wachangiaji wa mfuko huo.

Hayo yameelezwa na Kaimu Mkurugenzi Uendeshaji wa mfuko huo, Hamad Saleh Hamad, mara baada ya kuwasilishwa mpango huo kwa wadau kutoka taasisi mbali mbali za Serikali na binafsi, katika ukumbi wa Uhuru uliopo Kariakoo.

Alisema mpango huo unawataka wadau kutoa maoni yao ili mpango huo upate kutekelezeka vyema kwa muda uliowekwa.

Alisema maoni yatakayotolewa na wadau hao yataingizwa katika mpango mkakati uliopo ili kufikia malengo yaliyowekwa na mfuko huo.

Aliongeza kuwa mpango mkakati huo umezingatia dira ya maendeleo ya Zanzibar ya mwaka 2050, ilani ya uchaguzi wa Chama cha Mapinduzi pamoja na mpango wa kupunguza umasikini Zanzibar (MKUZA III).

Akiwasilisha mada juu ya mpango kazi wa miaka mitano ijayo, Iddi Juma Shaaban alisema, wamejipanga kuufanya mfuko huo kuwa endelevu ili wanachama wake wafaidike na si kufilisika.

Aidha alisema mpaka sasa bado kuna taasisi mbali mbali za serikali hazijawasajili wafanyakazi wao jambo ambalo linapeleleka mfuko huo kuwa na idadi ndogo ya wanachama.

Pia alisema kwa waliosajiliwa baadhi yao nao wamekuwa wakichangia viwango vidogo licha ya mfuko huo kuweka kiwango maalum.

Sambamba na hayo alisema ZSSF itaendelea kuangalia sehemu nyengine za uwekezaji kwa lengo la kuongeza mapato.

Aidha alisema watahakikisha kuwa wanatumia mifumo ya kisasa katika kutoa huduma ili waendani na kasi ya maendeleo na kutoa mafao kwa haraka licha ya kuwepo kwa baadhi wa wanachama huchelewa kupeleka baadhi ya taarifa.

Katika mpango huo pia watazingatia kutoa huduma bora kwa wanachama wake wote wa Unguja na Pemba.

Alisema kuufanya hivyo ni kuongeza wingi wa wanachama na ifikapo 2026 iwe imefikia asilimi 50 ambapo kwa sasa wapo asilimia 25 tu.

Miongoni mwa wadau walioshiriki katika mkutano huo Thabit Ali Nassor, kutoka Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale, ameishauri ZSSF kuangalia mifuko mengine jinsi inavofanya kazi kwa lengo la kupata maendeleo zaidi.

Pia aliutaka Mfuko huo kuacha kuwaimarishia maslahi wafanyakazi wao na badala yake washuke kwa wachangiaji juu ya namna gani watanufaika na Mfuko huo

Nae Mkurugenzi kutoka Ofisi ya Makamo wa Kwanza wa Rais, Daima Mohammed Mkalimoto, aliushauri mfuko huo kushirikiana na ofisi ya utumishi wa umma ili kupata wachangiaji zaidi.

Mshiriki kutoka Wizara ya Fedha na Mipango Maryam Yahya Ramadan, alisema mpango huo uliowasilishwa ipo haja kufikishwa katika wizara yao kwa lengo la kuupitia ili kupata taarifa zilizo sawa.