NA KHAMISUU ABDALLAH

KIJANA wa miaka 25 aliyedaiwa kumchinja mwenzake kidole, amepandishwa katika mahakama ya wilaya Mwanakwerekwe, kujibu tuhuma hizo.

Mshitakiwa huyo ni Abdalla Juma Omar mkaazi wa Melitano wilaya ya Magharibi ‘B’ Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, ambae alifikishwa katika kizimba cha Hakimu Fatma Omar.

Mwendesha Mashitaka, Wakili wa serikali kutoka Ofisi ya Mkurungenzi wa Mashitaka (DPP), Soud Said, aliiambia mahakama kwa kudai kuwa, mshitakiwa huyo alitenda kosa la shambulio la kuumiza mwili, ambalo ni kinyume na kifungu cha 230 cha sheria namba 6 ya mwaka 2018 sheria za Zanzibar.

Bila ya halali, alidaiwa kumshambulia Seif Suleiman Abdalla, kwa kumchinja na kisu katika kidole chake cha mwisho cha mkono wa kulia na sehemu ya mkono wa kushoto, kitendo ambacho kimemsababishia kupata maumivu, jambo ambalo ni kosa kisheria.

Tukio hilo alidaiwa kulitenda Mei 24 mwaka jana majira ya saa 6:50 za mchana huko Fuoni Mombasa wilaya ya Magharibi ‘B’ Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.

Mshitakiwa huyo aliposomewa shitaka hilo alilikataa na kuiomba mahakama impatie dhamana, huku upande wa mashitaka ukidai kuwa upelelezi wa shauri hilo tayari umeshakamilika na kuomba kupangiwa tarehe nyengine kwa ajili ya kusikilizwa.

Mahakama, ilimtaka mshitakiwa huyo kujidhamini mwenyewe kwa shilingi 500,000 za maandishi pamoja na kuwasilisha wadhamini wawili, ambao kila mmoja atamdhamini kwa kima hicho hicho cha fedha pamoja na kuwasilisha kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi na barua ya Sheha wa Shehia wanazoishi.

Hakimu Fatma, aliiahirisha kesi hiyo hadi Juni 3 mwaka huu na kuutaka upande wa mashitaka kuwasilisha mashahidi siku hiyo.

Mshitakiwa huyo alikamilisha masharti hayo na yupo nje kwa dhamana hadi tarehe nyengine aliyopangiwa mahakamani hapo.