ZASPOTI
MABINGWA watetezi, APR wamejikatia tiketi ya kucheza robo fainali ya ligi ya taifa msimu huu baada ya kupata ushindi wa 2-1 dhidi ya Bugesera FC kwenye Uwanja wa Huye.
Magoli ya APR yalifungwa na Yannick Bizimana na nahodha, Thierry Manzi kunako dakika ya 17 na 73 wakati bao la Bugesera lilitiwa kimiani na Jacques Ntwali kwenye dakika ya 55.

Miamba hiyo ya APR ilifuzu bila ya kupoteza mchezo hata mmoja wakiwa na pointi 12 kutokana na raundi nne wakati Gorilla iliifunga AS Muhanga 2-1 kwenye uwanja wa Muhanga na kujihakikishia pointi tisa katika mechi nne.

AS Muhanga na Bugesera FC wapo chini bila ya pointi kwenye kundi ‘A’.
Wakati huo huo, katika mechi nyengine za kundi, Kiyovu iliinyuka Gasogi United 4-1 wakati Rayon Sports ilibanwa sare ya 1-1 dhidi ya Rutsiro FC.
Mchezaji mpya, Heritier Nzinga Luvumbu aliifungia ‘Blues’ kunako dakika ya 25, lakini, Jean Claude Ndarusanze akasawazisha kwenye dakika ya 84.

Rayon inaongoza msimamo ikiwa na pointi saba ikifuatiwa na Kiyovu yenye pointi sita wakati Gasogi na Rutsiro zina pointi nne na michezo miwili iliyobakia katika kundi ‘B’.
AS Kigali na Polisi zinaongoza katika kundi ‘C’ zikiwa na pointi tisa wakati katika kundi ‘D’, Marines na Sunrise wapo mbele kwa pointi saba.

Timu mbili bora za juu zitatinga fainali kwa tiketi ya moja kwa moja kuiwakilisha Rwanda kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho msimu ujao. (Newtimes).