NA MARYAM HASSAN
HAMID Mohammed Seif (32) mkaazi wa Kilimahewa, anaetuhumiwa kwa kosa la kukashifu mtoto wa kike mwenye umri wa miaka saba, amenusurika kwenda rumande baada ya wadhamini wake kukamilisha masharti aliyopewa katika mahakama ya mkoa Vuga.
Wadhamini hao, walipelekea mshitakiwa huyo kushushwa kwenye gari la mahabusu na kwenda kusherehekea sikukuu ya Idid el- Fitri uraiani.
Hakimu Hamisuu Saaduni Makanjira, alimtaka mshitakiwa huyo kujidhamini kwa bondi ya shilingi 500,000 pamoja na kuwasilisha wadhamini wawili, ambao kila mmoja watasaini kima hicho hicho huku wakitakiwa kuwasilisha kopi ya kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi pamoja na barua ya Sheha.
Wakati Hakimu huyo anatoa masharti hayo, wadhamini wa mshitakiwa huyo walichelewa kufika mahakamani, jambo ambalo lililopelekea kupandishwa katika gari kuelekea mahabusu ya Chuo cha Mafunzo Kilimani.
Hamid alisomewa kosa lake na Mwendesha Mashitaka wa serikali, kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Anuar Khamis Saaduni, ambae alidai kuwa, mshitakiwa huyo alitenda kosa hilo Aprili 23 mwaka 2018 majira ya saa 10:00 za jioni, huko Kilimahewa wilaya ya Mjini mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.
Bila ya halali, alidaiwa kumkashifu mtoto wa kike mwenye umri wa miaka saba, kwa kumvua nguo zake za ndani na kumtia vidole katika sehemu zake za siri za mbele bila ya ridhaa yake, kitendo ambacho ni kosa kisheria.