GABERONE, BOTSWANA

BOTSWANA na Zambia zimefungua daraja la Kazungula, ambalo linajumuisha barabara na njia ya reli juu ya mto Zambezi ambao unaunganisha nchi hizo mbili na kituo cha mpaka mmoja.

Daraja hilo hadi kukamilika kwake limegharimu dola za Kimarekani milioni 259.3, ambalo lina urefu wa mita 923, linatarajiwa kuwezesha upatikanaji wa masoko ya kimataifa baada ya kuunganishwa na bandari kuu sambamba na kuboresha ufanisi wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

Rais wa Botswanan Mokgweetsi Masisi alisema daraja la Kazungula litafungua njia ya uimarishaji wa biashara, upatikanaji wa ajira na kukuza uchumi katika nchi za SADC. “Kwa jumla, hiyo itaharakisha sana mchakato wa ujumuishaji wa SADC, ambao tunafuatilia kwa nguvu.”

Nae Rais wa Zambia Edgar Lungu alisema daraja hilo linaonyesha uhusiano mzuri kati ya nchi hizo mbili.

“Mradi wa daraja la Kazungula ulistahili juhudi zilizofanywa na kwamba kupitia usafiri wa barabara katika daraja la Kazungula utaimarisha sana kwa sababu ya muda uliopunguzwa wa kusafiri pamoja na hatua bora za uwezeshaji wa biashara na shughuli za usimamizi wa mpaka kwa sababu ya ujumuishaji wa kituo kimoja cha mpaka,” alisema.

Lungu alikiri msaada wa kifedha kutoka kwa serikali za China, Korea Kusini, Japan na Benki ya Maendeleo ya Afrika namna ulivyofanikisha ujenzi huo.

Mradi wa Kazungula ulianza mwaka 2014 na kituo cha kipya cha mpakani kinatarajiwa kufanya kazi masaa 22 kwa siku.