MOGADISHU, SOMALIA

WABUNGE wa Somalia wamepiga kura kufuta nyongeza ya miaka miwili kwenye muhula wa rais Mohamed Abdullahi Mohamed Farmajo waliyoidhinisha mwezi uliopita baada ya kuzuka mvutano mkubwa wa kisiasa nchini humo.

Hatua ya bunge hilo kupitisha sheria ya kurefusha muda wa utawala wa rais Mohamed ilishuhudia kuzuka makabiliano kati ya pande hasimu za wanajeshi kwenye mkuu wa taifa hilo, Mogadishu.

Zoezi la kura kubatilisha sheria hiyo lilirushwa moja kwa moja na televisheni nchini Somalia na lilifanyika muda mfupi baada ya rais Mohamed kulihutubia bunge na kutangaza nia ya kuitisha uchaguzi wa bunge uliocheleweshwa.

Nyongeza ya muhula wa rais iliidhinishwa na Baraza la Wawakilishi mwezi uliopita lakini ilipingwa na Baraza la Seneti na kuzusha mzozo wa kisiasa uliozidi makali wiki iliyopita.

Katika hotuba yake baada ya kura ya bunge, waziri mkuu wa Somalia Mohamed Hussein Roble aliamuru wanajeshi kurejea kwenye makambi na wanasiasa kuacha kuchochea vurugu.

Roble pia aliandika kupitia ukurasa wake wa Twitter kuwa serikali itafanya mipango ya kuandaa uchaguzi hivi karibuni. Muhula wa rais Mohamed ulimalizika mwezi Februari lakini bila ya kuwepo kwa wabunge wapya, bunge la nchi hiyo lisingeweza kumchagua rais mpya.

Jaribio la rais Mohamed Abdullahi la kurefusha muda madarakani pia limewakasirisha wafadhili wa kigeni ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakiiunga mkono serikali yake kwa matumaini ya kurejesha uthabiti baada ya miongo mitatu ya vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyozuka tangu mwaka 1991.