NA AMINA AHMED

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Kusini Pemba, kimempitisha Himid Omar Ali, kuwa mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) baada ya kuchaguliwa kwa kura 37 kati ya 55 zilizopigwa katika uchaguzi huo.

Akizungumza baada ya kukamilika uchaguzi huo katika ukumbi wa Baraza la Mji wa Chake Chake, Mwenyekiti wa CCM Mkoa huo, Yussuf Ali Juma, alisema lengo la uchaguzi huo ni kuchagua kiongozi  atakaesaidia kukitetea, kukiimarisha na kukijenga  chama.

Alisema Halmashauri ya CCM mkoa huo inaamini mjumbe aliechaguliwa ndie atakaekisaidia chama hicho katika harakati zake za kisiasa.

“Sisi kama chama tumemuamini na dio sababu tumemchagua sio kwamba wagombea wenzake hawafai lakini katika uchaguzi kuna mmoja huwazidi wenzake, tunaimani ataitumikia nafasi hii katika chama ipasavyo,” alisema.

Katibu wa CCM Mkoa wa Kusini Pemba, Mohamed Ali Khalfan, alisema uchaguzi huo wa mara ya pili ni kuziba nafasi ya iliyokuwa wazi baada ya aliekuwa akishikilia kupata nafasi nyengine.

Abrahaman Mwinyi ambae alikuwa mjumbe, alichaguliwa kuwa Mbunge katika uchaguzi mkuu uliopita na hivyo kupoteza sifa ya kushikilia nafasi hiyo.

Awali akitangaza matokeo baada ya kukamilika kwa uchaguzi huo mbele ya wajumbe, Msimamizi wa uchaguzi, Salum Khatib Reja, ambae pia ni Katibu wa sekreterieti ya halmashauri kuu ya CCM Taifa, alisema wagombea walioomba nafasi hiyo walitumia vyema haki yao ya kikatiba ya kuomba nafasi hiyo.

Alisema kwa mujibu wa kura zilizopigwa katika uchaguzi huo, Himid Omar Ali, alipata kura 37 na kuwa mshindi.

Aliwataka wale wote ambao kura zao hazikutosha kuvunja makundi na hatimae kumpa ushirikiano mjumbe huyo.

Aidha katika uchaguzi huo pia CCM mkoa huo kiliwateua, Farhat Khamis Juma na Ali Nassor Mohammed kuwa wajumbe wa Halmashauri Kuu ya siasa mkoa huo.

Wagombea wengine walikuwa ni Mohammed Abdalla, Salum Khamis, Yussuf Hamad na Himid Omar Ali.