NA KHAMISUU ABDALLAH

CHAMA cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, kimemtaka Mwanansheria Mkuu wa Serikali ya mapinduzi Zanzibar kuhakikisha watu wote waliohusika katika wizi na upotevu wa fedha za serikali wanachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.

Katibu wa Kamati Maalum ya NEC, Idara Itikadi na Uenezi Zanzibar, Catherine Peter Nao, alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na vyombo vya habari Ofisini kwake Kiswandui, Zanzibar ikiwa ni siku tatu tokea Kaimu Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kukabidhi ripoti ya ukaguzi ya mwaka 2019/2020 kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi.

Alieleza kuwa ni jambo la msingi kwa kila mtu atakaebainika kufanya hivyo kuchukuliwa hatua kisheria na kusisitiza kuwa hatua hiyo itaongeza uwajibikaji na kupunguza kasoro katika kaguzi zinazofuata.

Alisema dosari zilizoainishwa katika ripoti ya ukaguzi wa CAG ni nyingi na upotevu wa fedha ungesaidia katika maendeleo ya nchi hivyo ni lazima hatua stahiki zichukuliwe ikiwa ni pamoja na kurudishwa kwa fedha hizo.

“CCM haitaki taarifa hiyo iishie katika makabati bali tungependa kusikia na kuona mamlaka zinazohusika zinachukua hatua ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, kuimarisha utawala bora na maendeleo ya Zanzibar na watu wake,” alieleza Catherine.

Aliongeza kuwa CCM imesosoneshwa na kitendo cha baadhi ya watumishi kukwamisha ukaguzi wa CAG katika taasisi zao na kusisitiza kuwa jambo hilo halikubaliki kisheria na kikatiba hivyo waliohusika wanapaswa kuwajibishwa.

“Haiwezekani katiba ya nchi inaanzisha ofisi ya Mkaguzi na inampa mamlaka ya kufanya kazi kwa maslahi ya nchi halafu wanatokeo watu wanakwambisha kazi yake kwa maslahi yao binafsi. Jambo hili limetuudhi na kutusikitisha, lazima tuwajibishane tusikubali kuishi kimazoea,” aliongeza Catherine.

Aidha aliwaomba wananchi kuumuunga mkono Rais Dk. Mwinyi katika vita dhidi ya ubadhirifu, rushwa na uhujumu uchumi na kuwaomba Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kuijadili taarifa hiyo kwa kina na kutoa mapendekezo yatakayochangia kuongeza tija na uwajibikaji.

“Tunaomba wakati utakapofikia, Wawakilishi waijadili ripoti ya CAG bila ya ushabiki, kipengele kwa kipengele na nini walichokiona ili hatua kali zichukuliwe kwa wahusika wote. Kwa hili tutakula sahani moja na ukizingatia idadi kubwa ya wajumbe wanatokana na chama cha CCM,” alibanisha.

Katika hatua nyengine, Katibu Catherine alisema CCM bado haijaridhika na kasi ya utendaji wa mawaziri, hivyo aliwaomba kuongeza kasi ya uwajibikaji ili matokeo na maagizo ya Rais yaonekane kwa haraka.

“Chama bado hakijaona hasa kasi ya kazi zinazofanywa na mawaziri hasa katika suala la kukutana na wadau husika kama agizo la Rais linavyowataka. Hoivyo tunawataka wafanye hivyo na waache kuibeza kauli ya kiongozi wao kwani wapo watu ambao wanakuja kutulalamikia sisi hapa ofisini kwetu hasa suala la kodi,” aliwasisitiza.

Alisema imani ya rais ni kuona maendeleo ya haraka yanafanyika ikiwemo kiuchumi kijamii na kimaendeleo hivyo ni lazima watendaji hao waende na kasi ili kufikia matarajio ya wananchi.

Kwa upande wa miradi kikubwa iliyoibuliwa na Rais katika uwekezaji, aliwaomba wanahabari kumsaidia katika kutoa vipindi maalum vya kuelimisha wananchi juu ya miradi hiyo ambayo itaweza kuwaamsha vijana katika kujiandaa katika kushiriki uchumi wa nchi yao hasa uchumi wa bluu.

Mbali na hayo, alimpomgeza Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan katika kuwaongoza watanzania kwa kipindi kifupi toka akabidhiwe madaraka hayo.

Chatherine alisema CCM itaendelea kuzisimamia serikali zote mbili za Tanzania na kuahidi kuwa wapo pamoja katika dua na sala katika uongozi wake na kuahidi kuwaelimsha wananchi juu maendeleo ya Zanzibar.