Wataka akimama wajawazito kujifungulia hospitalini

NA MOHAMMED SHARKSY (SUZA)

DUNIA leo inaadhimisha siku ya wakunga duniani ambapo Zanzibar kama sehemu ya dunia nayo inaiadhimisha siku hiyo muhimu kwa maisha ya akinamama wajawazito pamoja na watoto wachanga.

Siku hii ni muhimu kwa kuwa wazazi hasa wajawazito wanalazimika kupata huduma bora katika kipindi chote cha ujauzito sambamba na wakati wa kujifungua.

Aidha mara tu baada ya kujifungua hulazimika kuwa na uangalizi wa afya ya mama na mtoto kusudi kuona hakuna matatizo yanayowakumba watu hawa katika kipindi hicho.

Na ndio maana kauli mbiu ya siku hii ya ‘Fuatilia taarifa, wekeza kwa wakunga’ inasadifu namna ya kuipa umuhimu mkubwa afya ya mama na mtoto kwa kipindi hicho maalumu.

Kauli mbiu ya mwaka huu inahamasisha na kutaka juhudi endelevu zichukuliwe katika kuekeza kwa Wakunga kama msingi wa kukinga vifo vya mama na mtoto ili kufikia lengo no 3.1 la maendeleo endelevu (Sustainable Development Goal) la kupunguza vifo vya mama kwa chini ya vifo 70 kwenye mama hai 100,000 ifikapo 2030.

Aidha mwaka huu siku ya Wakunga Duniani inaadhimishwa pamoja na uzinduzi wa “Repoti ya Dunia ya Ukunga (State of the World’s Midwifery Report)” ambayo ni ushahidi wa kutosha juu ya nguvu kazi ya Wakunga duniani kote sambamba na taarifa inayohamasisha mijadala ya kisera na hatimaye kuleta mabadiliko ya kisera.

Kwa mujibu wa risala ya wakunga katika kilele cha siku hiyo ya maadhimisho Siku ya Wakunga Duniani inasherehekewa kila mwaka ili kuadhimisha na kuongeza uwelewa wa mchango wa Wakunga kwa jamii duniani.

Katika kuadhimisha siku hii, wakunga wamefanya shughuli mbali mbali katika hospitali za Zanzibar ikiwemo Hospital ya Makunduchi. Miongoni mwa shughuli hizo zikiwemo, huduma za uchunguzi wa awali wa mama baada ya kujifungua na usafi wa sehemu za kutolea huduma pamoja na eneo la hospitali.

Kutokana na takwimu mbali mbali imeonekana kwamba wanawake wapatao 295,000 hufa duniani kila mwaka kutokana na madhara yatokanayo na ujauzito au wakati na baada ya kujifunguwa.

Kwa mujibu wa wakunga, tafiti ya TDHS ya mwaka 2015/2016, kwa Tanzania inaonyesha wamama 556 kwenye mama 100,000 hufa kila mwaka, ripoti ya HMIS, 2017 ya Zanzibar, inaonyesha akimama 267 kwenye mama 100,000 hufa kila mwaka.

Aidha, watoto wachanga wapatao milioni 2 wanafariki mara tu wanapozaliwa au katika masaa 24 baada ya kuzaliwa, na watoto milioni 2.6 wanazaliwa wakiwa wafu duniani kote. Vifo hivi vingi hutokea katika nchi za kusini mwa jangwa la Sahara ikiwemo Tanzania na Zanzibar.

Vifo hivi vingeweza kuzuilika kwa kuongeza umakini wakati wa kutoa huduma za mama na mtoto, ambapo kwa mujibu wa ripoti ya (HMIS), Zanzibar tumefanikiwa kupunguza vifo vya kinamama kutoka 422/100,000 mwaka 2008 hadi 267/100,000 mwaka 2017 ambao hufa kutokana na sababu mbali mbali zikiwemo, kutokwa na damu nyingi baada ya kujifunguwa,magonjwa ya presha inayoambatana na ujauzito, kutokwa na damu nyingi kabla kujifunguwa na kifafa cha mimba.

Hali hizi huhitaji matibabu ya dharura, uwepo wa vifaa husika katika sehemu zote za kutolea huduma pamoja na wahudumu wa kutosha.

Hata hivyo idadi ya wajawazito wanojifungulia katika vituo vya afya imeongezeka kutoka 27,506 (sawa na asilimia 43.2) mwaka 2011 hadi 41,795 (sawa na asilimia 68.3) mwaka 2014 haya ni mafanikio kwetu.

Risala hiyo ya wakunga inaeleza kuleta mabadiliko chanya katika afya ya jamii, Siku ya wakunga duniani imeanzishwa kuongeza uelewa wa majukumu ya wakunga pamoja na kuona umuhimu wa kutimiza mahitaji ya wakunga duniani kote.

“Juhudi za pamoja zimeanzishwa katika uwepo wa wakunga wenye taaluma katika mifumo ya afya na utoaji huduma sambamba na upatikanaji wa vifaa kwa ajili ya huduma lakini bado haujatosheleza”, walisema wakunga katika risala yao.

Kwa mfano hapa Zanzibar, fani ya ukunga imeanza zamani sana na imekuwa ikiimarika siku hadi siku kutokana na umuhimu wake kitaifa na kimataifa. Hivi sasa idadi ya vituo vya afya vinavyotoa huduma ya kuzalisha vimeongezeka katika ngazi ya kijiji hadi kufikia vituo 58 mwaka 2021.

“Tunaipongeza Serekali kwa kuongeza vituo ili kupunguza wingi wa wajawazito wanaojifungulia hospitalini, hivyo tunaiomba jamii kutumia vituo hivyo, tunatowa shukrani zetu za dhati kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar pamoja na wadau mbali mbali wa Maendeleo kwa juhudi mbali mbali inazofanya katika kuhakikisha kada ya ukunga inaboreka.

Hii ni pamoja na kupatiwa ufadhili kwa wakunga na walimu wa ukunga kwenda kujiendeleza kielemu ambapo hadi hivi sasa kuna wakunga bingwa zaidi ya watano (5) ambao wamemaliza masomo yao katika vyuo mbali mbali nchini, pamoja na kuboreshwa kwa miundo mbinu ya utoaji huduma ikiwemo ujenzi na ukarabati wa majengo”, ilisema risala hiyo ya wauguzi.