NA PILI MWINYI, CRI

HAKUNA kitu chenye thamani duniani kama mtu kuwa na afya bora, kuwa na afya ndiko kunakomuwezesha mtu kupata nguvu ya kutekeleza shughuli zake mbalimbali ikiwemo kujitafutia riziki kwa ajili ya kujikimu kimaisha.

Ni kama msemo wa Kiswahili unavyosema “Bora afya kuliko mali”, yaani ukiwa na mali wakati afya yako imezorota inakuwa haina faida yoyote.

China imefanya maamuzi makubwa na kuweka malengo ya kuijenga jamii yenye afya bora, ambapo mnamo mwaka 2016, ilitoa waraka wa uliopewa jina la ‘China yenye Afya 2030’.

Waraka huo unaelezea mipango na mikakati ya serikali katika kuhakikisha inavyofanikisha kuipatia afya bora jamii ya nchi hiyo hadi kufikia mwaka 2030.

Mpango huo umeanza kutekelezwa 2019, ambapo pamoja na mambo mengine kuna mikakati ya kutatua shida za upatikanaji wa huduma za afya na kujitahidi kuhakikisha zinawafikia watu.

Rais Xi Jinping aliwahi kusema kwamba, “Haiwezekani watu wote kuwa na ustawi bila ya watu wote kuwa na afya”. Kwa hiyo maneno haya moja kwa moja yanahimiza mamlaka husika kuweka kipaumbele kwenye kuimarisha huduma za afya kuanzia ngazi ya mashinani.

Aidha kuhimiza upatikanaji sawa wa huduma za umma za msingi mijini na vijijini na kuwapatia watu huduma rahisi, salama, zenye ufanisi na watakazomudu za afya.

Tukichukulia mfano wa kisiwa kidogo cha Shiye, cha China, kilichozungukwa na maji ya mto Yangtze ambacho ni vigumu kukifikia.

Zamani wakazi wa kisiwa hicho sio tu walikuwa na hofu ya kuugua bali waliogopa hata kusafiri nje ya kisiwa hicho kwasababu ya mawasiliano duni na nje ya kisiwa.

Lakini mabadiliko makubwa yanaonekana sasa, baada ya rais Xi kufanya ziara ya ukaguzi mwaka 2014 kwenye mji huo. Hivi sasa, watu hawana haja tena ya kuondoka kwenda nje ya kisiwa kutafuta matibabu hata kwa magonjwa madogo.

Katika miaka kadhaa iliyopita vimeshuhudiwa vitengo vitano, vikiwemo vya magonjwa ya moyo na kisukari vikianzishwa kwa ushirikiano wa pamoja na zahanati ya mji wa Shiye na hospitali za huduma za afya za mji wa Zhenjiang.

Zahanati hiyo sasa ina vifaa vya kisasa vya kupimia magonjwa kwenye kila kitengo, huku watu wake wakifurahia huduma za matibabu zinazotolewa na hospitali za mji huo.

Huu ni mfano mmoja tu kwa hapa China, mabadiliko mengi yameshuhudiwa baada ya rais mwenyewe kufanya ziara za ukaguzi kwenye maeneo mbalimbali ya nchi.