NA KHAMISUU ABDALLAH

SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar, imesema itaendelea kuthamini mchango unaotolewa na Jamhuri ya watu wa China kupitia sekta mbali mbali za kimaendeleo na kijamii ikiwemo afya.

Waziri wa Fedha na Mipango Zanzibar, Jamal Kassim Ali, alisema hayo wakati mazungumzo yake na Balozi mdogo wa China nchini Tanzania aliyepo Zhang Zhisheng, ofisni kwake Vuga, mjini Unguja.

Alisema China imekuwa ikisaidia kwa kiasi kikubwa Zanzibar hasa kwenye sekta ya afya ikiwemo ujenzi wa hospitali ya Abdalla Mzee kisiwani Pemba na hata kuleta madaktari bingwa.

Waziri Jamal, alibainisha kuwa mbali na sekta ya afya, China pia inasaidia udhamini wa masomo kwa wafanyakazi mbali mbali wa taasisi za serikali na kuiomba kuendelea kusaidia nafasi hizo.

Aidha alisema mazungumzo hayo yamelenga katika kuendelea ushirikiano huo ikiwemo ujenzi wa nyumba za makaazi kwa madaktari katika hospitali ya Abdalla Mzee kisiwani Pemba.

Hata hivyo, alibainisha kuwa mambo mengine waliyoomba kwa serikali ya China ni namna gani watasaidia katika suala la barabara na vituo vya ICT katika tasisi za elimu Unguja na Pemba.

“Tumeoma angalau kituo kimoja kikubwa cha ICT kiwe Pemba na kimoja Unguja vitakavyoweza kutoa fursa kwa ICT kwa watumiaji watakaokuwa ndani ya vyuo na umma kwa ujumla.

Aidha Jamal alibainisha kuwa jambo jengine ni kuona namna gani China itakavyoshiriki katika uchumi wa bluu hasa katika ujenzi wa Bandari ya Mangapwani ya ambao tayari mpango wa ujenzi wa bandari hiyo umeshawasilishwa serikalini na hatua iliyobaki ni kuwapata watu watakaojenga bandari hiyo.

“Tumeewambia wenzetu wakati utakapofika wasisite kushiriki katika mchakato huu kwani China ni marafiki zetu wa siku nyingi tokea Mapinduzi mpaka leo,” alibainisha.

Alisema anaamini kwamba Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Serikali ya China zitaendelea kusirikiana kwa maslahi ya nchi zao kwani uhusiano wao kwani China ni mdau muhimu kwa maeneleo ya Zanzibar.

Kwa upande wake Balozi Zhang, alisema uhusiano uliopa kati ya China na Zanzibar ni wa muda mrefu ambao umeleta tija kwa nchi zote mbili.

Aliahidi na kuahidi kuwa nchi yake itaendelea kushirikian na kusaidia shughuli mbali mbali za maendeleo ya Zanzibar na wananchi wake na kukuza uchumi wake kupitia sekta ikiwemo uchumi wa bluu ili Zanzibar ipige hatua kubwa kimaendeleo.