NEW DELHI, INDIA
WIZARA ya afya nchini India imesema taifa hilo la Kusini mwa Asia limerekodi maambukizi mapya zaidi ya 350,000 ndani ya saa 24 zilizopita na kufikisha idadi jumla ya watu walioambukizwa kufikia milioni 18.3
Ikiwa na maambukizi mapya 379,257 India, kwa sasa imeripoti visa zaidi ya milioni 18.3 vya maambukizi ya virusi vya corona ikichukua nafasi ya pili ya taifa lililo na idadi kubwa ya maambukizo baada ya Marekani.
Taarifa ya wizara hiyo iliripoti vifo 3,645 ndani ya saa 24 zilizopita na kufikisha idadi jumla ya watu waliofariki kutokana na ugonjwa wa COVID-19 kufikia 204,832.
Aidha taarifa hizo ziliongeza kuwa kwa siku saba mfululizo India imerekodi maambukizi mapya zaidi ya laki tatu na nusu kila siku hali inayopelekea mfumo wake wa afya kuendelea kulemewa na kusababisha mataifa ya nje kutuma misaada ya haraka.
Kulingana na wataalamu, taifa hilo la Kusini mwa Asia lililo na idadi ya watu bilioni 1.4 halikufikiria kuwa litaelemewa baada ya maambukizi kupungua mwezi Septemba, lakini kutokana na mikusanyiko ya watu wengi, hasa katika mikutano ya kisiasa,
Sherehe za kidini na watu kutochukua tahadhari ya kujikinga pamoja na matamshi ya viongozi wanaojisifu kuwa India imeshhinda vita dhidi ya virusi hivyo na ndio sababu zinazosemekana kusababisha taifa hilo kukumbwa na makali ya corona. Aina mpya ya kirusi cha corona pia kinasemekana kuchangia ongezeko hilo.