NA ABDUL-WAHID ABDU

MKUU wa wilaya ya Kusini, Rashid Makame Shamsi amemtaka muwekezaji Hans Ullrich wa Ndame Beach hoteli iliyopo Paje kuhamisha mali zake zilizopo katika hoteli hiyo kufuatia kumalizika kwa mkataba baina yao na wamiliki wa hoteli hiyo.

Tamko hilo alilitoa huko Paje mara baada ya kufika katika eneo la hoteli hiyo kwa lengo la kumsimamisha muwekezaji huyo ambaye ametakiwa kuondoka katika eneo hilo kufuatia barua iliyotolewa kutoka kamisheni ya utalii inayomtaka kusimamisha shughuli za uwekezaji katika hoteli hiyo.

Rashid alisema kuwa ni vyema muwekezaji huyo kufuata sheria na taratibu zilizowekwa ikiwemo kuondoka katika eneo na kuiwachia familia ambayo ndio wahusika wa mali hiyo.

Aidha mkuu huyo aliwataka wawekezaji wengine kufuata sheria na taratibu za nchi pamoja na kufuata maagizo ya wamiliki wa maeneo wanayowekeza ili kuepusha migogoro kama hiyo.

Kwa niaba ya wamiliki wa hoteli hiyo, Ali Suleiman Waziri ambae ni mwanafamilia ya Ndame, alisema kuwa hawakuridhishwa na uendeshaji wa hoteli hiyo ambayo kwa sasa hairidhishi mazingira yake pamoja na uchakavu wa majengo yake.

Hata hivyo wanafamilia hao walisema kuwa tayari mkataba na muwekezaji huyo umekwisha hivyo hakuna haja ya muwekezaji huyo kuendelea kubakia katika eneo lao.

Sambamba na hayo pia wanafamilia walimshukuru waziri mwenye dhamana ya utalii na mkuu wa wilaya kwa kusimamia vyema majukumu yao yanayokwenda na kasi ya awamu ya nane ya Dk. Hussein Ali Mwinyi inayohitaji uwajibikaji, usawa na kasi ya uchumi wa buluu.