MARYAM HASSAN NA HUSNA SHEHA

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi, Dk. Khalid Salum Mohammed, ameeleza kuwa suala la mfuko wa pamoja wa fedha za muungano ni miongoni mwa mambo yanayoshughulikiwa serikali zote mbili hivyo wananchi wanapaswa kuwa wavumilivu.

Dk. Khalid alisema hayo wakati akitoa ufafanuzi wa hoja za wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, waliochangia hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi yake kwa mwaka wa fedha 2021/2022 katika mkutano wa tatu wa baraza hilo unaoendelea mjini Zanzibar.

Alisema asilimia 4.5 ya mgao wa fedha kutoka Benki Kuu ya Tanzania na mashirika ya taasisi za muungano unategemea na makubaliano ya serikali mbili ambazo bado zinaendelea kulifanyia kazi.

Alisema suala hilo ni fomula ya muda ambayo iliwekwa hadi pale serikali zote mbili zitakapokubaliana juu  ya mapendekezo ya tume ya fedha ya pamoja.

Kuhusu suala la ajira za kwa taasisi za muungano, alisema kupitia kamati ya SMT na SMZ inayoshughulikia changamoto za muungano zimefikia muafaka wa kuwa na mgao wa asilimia 21 kwa Zanzibar na asilimia 79 kwa upande wa Tanzania bara.

“Katika makubaliano yaliyowekewa waajiriwa wa pande zote mbili lazima wawe na vigezo vinavyohitajika kutokana na ajira inayokusudiwa,” alisema Dk. Khalid.

Akizungumzia kuhusu utekelezaji wa mradi wa TASAF, alisema hivi sasa serikali inataka kwenda kwenye awamu ya pili TASSAF III awamu ya pili inakusudia kuziingiza shehia zote za Unguja na Pemba.

Alisema awamu ya kwanza ilikuwa inachagua baadhi ya shehia, hivyo alifahamisha kuwa wale wote wenye vigezo watakuwemo katika mpango wa kunusuru kaya masikini.

Aidha Dk. Khalid aliwataka wananchi kujitokeza kwa wingi ili kuondosha malalamiko ya kutolewa katika mradi huo, kwa sababu sasa wanaendelea kufanya uhakiki.

“Katika uhakiki huu wale wote ambao hawana sifa na waliingia kwa bahati mbaya uhakiki itabidi uwatoe, tunataka wale wanaostahiki kwa mujibu wa vigezo vilivyowekwa,” alisema.

Aidha alisema katika suala hilo hakutokuwa na ubaguzi , iwe kwa itikadi ya kisiasa, dini, rangi, kabila na hata katika eneo mtu anaetoka, muhimu wataangalia vigezo vilivyoweka.

Mapema wajumbe wa Baraza na Wawakilishi wamesikitishwa juu ya kuwepo kwa ubaguzi katika utoaji wa fedha za mradi wa kunusuru kaya masikini.

Mwakilishi wa jimbo la Wingwi Kombo Mwinyi Shehe alisema suala hilo limegubikwa na ubaguzi mkubwa katika kuwaibua watu husika.

“Kuna watu hawastahiki kupewa fedha hizi kwa mujibu wa hali zao, ambapo zoezi hilo limelenga kupewa watu wenye hali dhaifu, lakini utamkuta mtu anakwenda pale halingani na ule mradi uliowekwa,” alisema.

Nae Zainab Abdalla Salum, Mwakilishi wa viti maalum wanawake alisema bado kipo kitendawili katika masuala ya udhalilishaji licha ya kuundwa kwa mahakama.

Alisema changamoto kubwa ni suala la ushahidi wananchi bado hawajawa tayari kutoa ushahidi, pamoja na kuchelewa kutolewa kwa mafaili katika ofisi ya Mkurugenzi wa mashitaka.

Katika kikao hicho wajumbe wa baraza la wawakilishi wameipitisha jumla ya shilingi 89,030,482,044 kwa kazi za kawaida na kazi za maendeleo kwa mwaka wa fedha 2020/2021.