NA RAYA HAMAD, OMKR
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Dk. Saada Mkuya Salum, amesema uzoefu, heshima na nidhamu ni miongoni mwa vichocheo muhimu vinavyochangia kupatikana ufanisi.
Waziri huyo alieleza hayo huko ofisini kwake Migombani mjini Zanzibar kwenye hafla fupi ya kumuaga aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kitaifa ya Kuratibu na Udhibiti wa Dawa za Kulevya, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Jeshi la Polisi Kheriyangu Mgeni Khamis.
Dk. Mkuya alisema heshima, nidhamu na uzoefu wa mkurugenzi huyo aliokuwa nao wakati akiiongoza taasisi hiyo kwa kiasi kikubwa kumepatikana mafanikio na mabadiliko ya kuutendaji.
Alisema ujasiri na kujiamini kwa Kheriyangu akiwa mkuu wa taasisi hiyo, kumesababisha watendaji kuwa tayari muda wote katika kutekeleza majukumu yao katika kudhibiti dawa za kulevya.
Aidha waziri huyo alimshukuru Kheriyangu kwa utumishi wake na namna alivyosimamia taasisi yake pamoja na kuwashughulikia vyema vijana walioachana na matumizi ya dawa za kulevya.
“Kumtoa mtu katika mazingira hatarishi ya matumizi ya dawa za kulevya na ukamtengeneza akarudi hatika hali yake ya awali na kuanza kuaminiwa na familia sio jambo la masihara”, alisema Dk. Saada.
Kwa upande wake, katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Khadija Khamis Rajab alizipongeza jitihada zilizochukuliwa namkurugenzi huyo na kumuomba kuendelea kutoa ushirikiano na ushauri pale panapohitajika.
Akitoa shukurani kwa viongozi wakuu na wakuu wa taasisi zinazosimamiwa na Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kitaifa ya Kutaratibu na Udhibiti wa Dawa za Kulevya Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Jeshi la Polisi Kheriyangu Mgeni Khamis, alisema mashirikiano aliyoyapata yamemuwezesha kufanya kazi zake kwa ufanisi.
Kheriyangu alisisitiza kuwa maamuzi yote aliyokuwa akiyatoa yalikuwa yanapitia kwenye vikao kazi kwa pamoja jambo ambalo limeiwezesha Tume hiyo kupata mafanikio katika utendaji.
Aidha alisema amejifunza mengi ikiwemo maisha ya kijamii kwa vile wakati anateuliwa mwaka 2013 alikuwa anatokea kwenye jeshi la polisi, jambo hili litamsaidia kufahamu namna ya kupambana na wahalifu wakati wa kuendelea na majukumu yake katika jeshi la polisi kwa vile tayari anamtandao mzuri na wanajamii.
Nae Mkurugenzi Mtendaji mpya Tume ya Kitaifa ya Kuratibu na Udhibiti wa Dawa za Kulevya, Luteni Kanal Burhani Nassoro aliahidi kushirikiana na watendaji na wafanyakazi ikiwa ni pamoja na kuendeleza mazuri yote yaliyoachwa na mtangulizi wake.
Akitoa shukurani kwa niaba ya wakurugenzi na wafanyakazi Mkurugenzi Mtendaji Tume ya UKIMWI Zanzibar, Dk. Ahmed Mohamed Khatib alimshukuru mkurugenzi anaeondoka na kusema kuwa ameacha alama ya upendo na nidhamu iliyodumisha maelewano kwa watendaji na wafanyakazi.
Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais imemzawadia cheti cha shukurani pamoja na zawadi nyengine ikiwa ni kuonesha kudhamini kazi nzuri aliyoifanya wkati akiiongoza taasisi hiyo.
Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Jeshi la Polisi Kheriyangu Mgeni Khamis aliteuliwa mwaka 2013 kuitumikia tume hio hadi Aprili 2021 ambapo anakwenda kuendelea na majukumu mengine ya kazi.