‘Upigwaji mkubwa’ wabainishwa
Aahidi hatua kali kwa waliokaanga mbuyu
NA KHAMISUU ABDALLAH
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema hatokuwa tayari kuonekana anashindwa kutekeleza wajibu wake hasa katika suala la udhibiti wa mapato ya serikali na kusisitiza kwamba atawachukulia hatua wale wote waliohusika na upotevu wa mapato.
Dk. Mwinyi alitoa kauli hiyo jana mara baada ya kupokea ripoti ya Mdhibiti na mkaguzi Mkuu wa hesabu za serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa mwaka 2019/2020 ikulu Mjini Unguja.
Alisema atakapoipokea ripoti ya mwakani hatokuwa tayari kuona kuna kasoro zilizobainika katika ripoti hiyo kwani kujitokeza kwa kasoro maana yake wameshindwa kutekeleza wajibu akiwemo yeye, mawaziri na makatibu wakuu.
Alisema kila mmoja wakiwemo mawaziri na makatibu wakuu ndio wasimamizi wakuu wa suala hilo na kuwaeleza kuwa baadhi ya mashirika ambayo yapo chini yao na taasisi hawawezi kusema kama hawahusiki na jambo hilo.
“Huwezi kusema huhusiki kama uwajibikaji ni lazima uanze juu ndio ushuke chini hivyo nitafurahi kusikia mtu fulani nimemfukuza au nimemsimamisha kazi au unamleta kwangu nichukue hatua kwa sababu ya hili hili, sasa sitofurahi kusikia mtu kafanya makosa yupo chini ya taasisi yako halafu unakaa kimya huwezi kuepuka lawama katika hili,” alisisitiza.
Dk. Mwinyi alisisitiza kuwa pamoja na kuwa ripoti hiyo waliyopokea wengi wao wameikuta lakini katika siku za usoni kila mmoja atawajibika moja kwa moja.
Alisisitiza kuwa atahakikisha anachukua hatua kali dhidhi ya wote waliohusika na upotevu wa mapato ili jambo hilo lisijirudie tena.
Aidha alisema ikiwa serikali itaendelea na utaratibu huo basi hawawezi kufika kwani kuna miradi mingi ya maendeleo na huduma za kijamii ikiwemo elimu, maji na afya hivyo wakiruhusu fedha hizo zote zipotee hawatoweza kufika.
Aidha alisema ni ukweli kuwa kuna upotevu mkubwa wa pesa za serikali kwani imeoneshwa na kubainishwa katika ripoti hiyo hasa upotevu katika makusanyo kwa taasisi zilizopewa jukumu la kukusanya bado upotevu ni mkubwa.
“Upotevu wa pesa za serikali ni mkubwa sana unaotokana na uhafifu wa mifumo na dhamira ovu kwa baadhi ya watendaji,” alisema.
Hata hivyo alibainisha kuwa sio katika suala la ukusanyaji pekee hata katika suala la matumizi ambapo pia kumeonekana upotevu kutokana na kutotumika vizuri.
Alisema lengo na madhumuni ya kupokea ripoti hiyo hadharani ni suala zima la kuhimiza uwajibikaji na utawala bora na kwamba ripoti hiyo inawataka kutafakari nini cha kufanya ili kudhibiti hali hiyo.
“Tutakuja kuzungumza kwa kina ili tuone hatua gani za msingi tuzichukue hatuwezi kusema kama tumepokea yamekwisha la tumepokea kwa lengo la kuchukua hatua madhubuti,” alibainisha.
Dk. Mwinyi alisema ni lazima serikali iwe wazi, kutambua changamoto ili kukabiliana na matatizo ambayo yalibainishwa katika ripoti hiyo.
Mbali na hayo, Dk. Mwinyi, alisikitishwa na kitendo cha mfanyakazi wa serikali kufikia kiwango cha kumzuia mkaguzi mkuu kutekeleza wajibu wake kwani jambo hilo haliwezi kuruhusiwa kwani kitendo hicho ni kuvunja katiba, sheria na kutowajibika.
Rais Mwinyi alimuagiza mkaguzi mkuu kuendelea pale aliposimamishwa kuanzia leo na kuwataka wahusika wote kutoa ushirikiano wa asilimia 100.
“Nisisikie tena fulani kazuia na waliokuwa hawapo kama mtu yupo likizo au amestaafu kwenye hili ni lazima arudi atoe maelezo kwa mkaguzi mkuu ni lazima tufike chini kujua mkaguzi amesimamishwa ameshabaini upotevu wa zaidi ya shilingi bilioni tano ambazo hazina maelezo,” alisema.
Alisema kwa mujibu wa katiba na sheria ana wajibu kuikabidhi rasmi ripoti hiyo Baraza la Wawakilishi kwa ajili ya kuchangiwa na kutoa maoni yao.
Hata hivyo, alisema aliipongeza ofisi hiyo kwa kazi nzuri walioifanya ambayo imebainisha changamoto nyingi na kuahidi kuzifanyia kazi changamoto zilizobainishwa katika ripoti hiyo.
Alikabidhi ripoti hiyo kwa viongozi mbalimbali akiwemo Makamu wa Kwanza wa Rais Othman Masoud Othman, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Hemed Suleiman Abdalla, Katibu Mkuu Kiongozi Mhandisi Zena Ahmed Said kwa ajili ya wafanyakazi wa serikali, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili anaesimamia shughuli za Baraza la Wawakilishi Dk. Khalid Salum Mohammed.
Akiwasilisha ripoti hiyo yenye vitabu sita vilivyojumuisha vitabu 169, Kaimu Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa hesabu za serikali (CAG), Dk. Othman Abass Ali, alisema katika ukaguzi alioufanya amebaini kasoro mbali mbali za kiutendaji na udhibiti wa mapato.
Alisema ofisi hiyo pia imefanya ukaguzi maalum kuhusu maagizo ya Rais aliyoyatoa alipowaapisha viongozi wakuu iliyojumuisha ripoti nane ikiwemo ripoti ya Shirika la Meli na Uwakala Zanzibar, malipo ya wazee pencheni jamii na utekelezaji wa miradi ya maendeleo hususan mradi wa pilipili hoho.
Ripoti nyengine zilizowasilishwa ni ripoti ya ukaguzi maalum kuhusu malipo ya fidia kwa wananchi walioathirika kupisha mradi wa uwekezaji wa ujenzi wa bandari, bohari na miundombinu ya mafuta na gesi Mangapwani na Bumbwini ambapo alibaini uwepo wa malipo kwa watu wasiohusika.
“Ripoti nyengine ni ya ukaguzi maalum kuhusu ununuzi wa mchele na mbolea uliofanyika wizara ya kilimo, ripoti ya ukaguzi maalum inayohusu ukodishwaji wa mashamba ya mikarafuu kisiwani Pemba, ripoti ya ukaguzi maalum kuhusu mfuko wa uwezeshaji wananchi kiuchumi kisiwani Pemba na malipo kwa nauli za walimu kisiwani Pemba,” alibainisha CAG.
Aidha Dk. Othman, alizitaja taasisi zililopata hati zenye shaka kwa kwa mwaka 2019/2020 ni pamoja na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Shirika la Biashara la Taifa (ZSTC), Shirika la Nyumba, Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA) na Mamlaka ya Mafunzo ya Amali (VTA).
Kwa upande wa serikali za mitaa, Dk. Othman alizitaja taasisi zilizopata hati zenye mashaka kuwa ni pamoja na Baraza la Manispaa Mjini, Baraza la Manispaa Magharibi ‘A’, Baraza la Manispaa Magharibi ‘B’, Baraza la Mji Kaskazini ‘B’, Halmashauri wilaya ya Micheweni, Baraza la Mji Chake Chake na Baraza la Mji Mkoani.
Kwa upande wa taasisi zilizopata hati mbaya kabisa alisema kwa upande wa mashirika ya umma na taasisi zinazojitegemea ni Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA) na Mamlaka ya serikali za mitaa ni Baraza la Mji Kaskazini ‘A’.
Akizungumzia matokeo ya ukaguzi kwa mwaka huo Dk. Othman, alisema serikali ilikadiria kukusanya shilingi tirioni 1.419.444 ambapo hadi kufikia Juni 30 mwaka jana jumla ya shilingi bilioni 983,461,584 zimekusanywa sawa na asilimia 69. 28 ya makadirio ikiwa na upungufu wa bilioni 485,982,416 sawa na asilimia 30.72.
Kwa upande wa mapato yatokanayo na kodi, alisema serikali ilikadiria kukusanya shilingi bilioni 859 na milioni 700 kwa mapato yatokanayo na kodi ambapo hadi kufikia Juni 30, 2020 mapato halisi yalikuwa ni shilingi bilioni 675,461 sawa na asilimia 78.6 ya makadirio na upungufu wa shilingi bilioni 184,239 ambapo serikali imeshindwa kufikia lengo la ukusanyaji wa mapato yaliyokadiriwa kwa asilimia 21.4.
Kwa upande mapato yanatokana na mashirika na taasisi za serikali, shilingi bilioni 107 na milioni 300 zikikadiriwa kukusanywa ikiwa ni makusanyo yasiyo ya kodi ambapo hadi kufikia Juni 30, makusanyo halisi yalikuwa ni shilingi bilioni 100 milioni 740 sawa na asilimia 93.9 ya makadirio tofauti ya shilingi bilioni 6 milioni 560 sawa na asilimia 6.4.
Kwa upande wa matumizi, alisema serikali ilikadiria kutumia shilingi tirioni 1 bilioni 419,444 kwa mwaka wa fedha 2019/ 2020 kati ya hizo shilingi bilioni 842 milioni 400 fedha kwa ajili ya kazi za kawaida na shilingi bilioni 577 na milioni 44 kutumika kwa kazi za maendeleo ambapo hadi kufikia Juni 2020 serikali ilitumia shilingi tirion 1 bilioni 19 milioni 776 sawa na asilimia 71.8 ya makadirio.
Alisema kati ya fedha hizo shilingi bilioni 722 milioni 618 zilitumika kwa kazi ya kawaida sawa na asilimia 85.79 na shilingi bilioni 297 milioni 158 zilitumika kwa kazi za maendeleo sawa na asilimia 51.49 ya makadirio.
Akizungumzia muundo wa gawio la serikali alisema kwa mwaka huo serikali ilikadiria kupokea gawio bilioni 17 na milioni 500 ikiwa ni gawio kutoka mashirika mbalimbali yanayomilikiwa na serikali ambapo hadi kufikia Juni 30 mwaka jana makusanyo halisi yalikuwa ni shilingi bilioni 16 milioni 855,970.
Alibainisha kuwa katika ripoti hiyo kwa ujumla ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa hesabu za serikali imebaini upotevu mkubwa wa pesa za serikali katika Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB) kutokana na kutofanya kazi kwa mifumo ya kifedha na kulipwa fidia kwa watu wasiohusika katika mradi wa ujenzi wa bandari ya Mangapwani.
Kasoro nyengine alisema ni upungufu wa uwasilishwaji hesabu jumuishi kwa mawazira na mashirika ya umma kwa kutozingatia mwaka wa fedha, kukosekana kwa nambari ya vifungu vya bajeti, mchanganuo wa mapato unaotokana na kodi.
Jengine ni kutojumuishwa kwa taarifa za fedha kwa taasisi mbalimbali, upotevu wa fedha katika ujenzi wa uwanja wa ndege Kigunda, kutokuwepo kwa makusanyo halisi kwa taasisi za umma na mashirika ya serikali, ukiukwaji wa sheria katika manunuzi na kulipa mishahara hewa kwa wafanyakazi ambao hawapo kazini kwa kipindi kirefu.