Ahimiza uwajibikaji kuimarisha maendeleo
Alitaka baraza la vijana kuzungumzia changamoto zinazowahusu
NA KHAMISUU ABDALLAH
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amewataka vijana kutunza amani na kuwaasa kutokubali kutumiwa na watu ambao hawaitakii mema nchi yao.
Dk. Mwinyi alitoa kauli hiyo katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Makamu wa Pili wa Rais, Hemed Suleiman Abdullah, katika ufunguzi wa mkutano na uchaguzi mkuu wa Baraza la Vijana Zanzibar uliofanyika katika ukumbi wa mitihani wa skuli ya Bubwini, wilaya ya Kaskazibi ‘B’, Unguja.
Alisema Zazibar ni nchi ya amani na kubainisha kuwa ni rahisi kuivunja amani na vigumu kuirudisha iliyotoweka hivyo ni lazima kila mmoja kuhakikisha anailinda amani ya nchi yao ili kupata maendeleo.
Alisema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ilipoamua kuanzisha chombo hicho kupitia sheria namba 16 ya mwaka 2013, ilidhamiria kukihalalisha na kukipa uwezo wa kufanya kazi zake kwa mujibu wa sheria.
Dk. Mwinyi alisema chombo hicho pia kilizingatia changamoto na mapendekezo yote yanayowahusu vijana yanazungumzwa na kufikishwa sehemu husika kwa wakati muafaka.
Alisema baraza hilo ni jukwaa lilaotengeneza vijana kuwa wazalendo wa nchi yao kuwafinyanga kuwajenda na kuwaanda vijana kuwa viongozi bora wa baadae na kuwahamisha ili waweze kujitolea bila ya kuangalia maslahi yao binafsi.
Aidha alisema serikali inatambua ukubwa wa tatizo la ajira ambalo kwa mujibu wa utafiti wa nguvu kazi Zanzibar ni asilimia 21.3.
Alisema kwa kutambua tatizo hilo, serikali imechukua hatua kupunguza tatizo hilo kwa kubuni na kutekeleza program mbalimbali za kupambana na tatizo hilo ikiwemo za mafunzo ya amali na mfuko wa uwezeshaji wananchi kiuchumi.
Alisema Zanzibar inakabiliwa na matumizi ya dawa za kulevya, ongezeko la maambukizi mapya ya VVU na Ukimwi na ongezeko la vitendo ya udhalilishaji ambapo asilimia kubwa ni vijana hivyo ni lazima vijana kwa umoja wao kutekeleza mapambano juu ya vitendo hivyo.
Hata hivyo aliwaomba wajumbe wa mkutano huo kuchagua viongozi waaminifu, waadilifu, wazalendo, wanaojielewa wenye wenye nidhamu, tabia, maadili mema,wanaouzika na wenye uwezo wa kupambanua mambo ili waweze kuliongoza baraza hilo.
Katika hatua nyengine aliwasihi viongozi watakaochaguliwa kuzingatia majukumu yao na kutoliendesha baraza hilo kwa maslahi na utashi wao wao binafsi na kuwasisitiza kuisoma sheria na kanuni za baraza hilo kwa ufanisi mkubwa.
Nae Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Tabia Maulid Mwita, alisema wizara imejipanga katika kuhakikisha ajenda ya vijana inakuwa namba moja katika masuala yanayoisaidia serikali kufikia maendeleo iliyojipangia.
Alisema alisema vijana ni muhimu katika nchi kwani ikiwa wataweza kuwasaidia mapema katika kutekeleza ilani ya CCM basi anaamini kwamba itakapofika uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 itakuwa haina kazi ya kuomba kura.
Hata hivyo alibainisha kuwa wizara imejipanga vizuri kwa kusimamia mambo yote ambayo wameekewa kwa mujibu wa kanuni na utaratibu na kusisitiza kuwa inapokwenda katika ajenda ya vijana haitaki mchezo.
Mbali na hayo alisema wizara ipo katika mchakato wa mapitio ya sera ya vijana kuhakikisha wanangalia changamoto zilizokuwepo na kuiboresha ili iweze kuendana na wakati na mahitaji ya vijana na wakati uliopo katika kufikia utekelezaji wa ilani yam waka 2020/2025.
Sambamba na hayo aliwaisihi vijana kuwa tayari katika uchumi wa bluu na viwanda kwani unaowahusu zaidi wao ambao ndio nguvu kazi ya leo hivyo aliwaomba kushirikiana pamoja katika kufikia malengo ya serikali katika kutoa fursa ya ajira.
Mapema Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Zanzibar, Khamis Rashid Kheir (Makoti), aliishukuru serikali kuanzisha chombo hicho kwani zipo nchi ambazo hawana chombo hicho.
Aliipongeza serikali kwa kulisaidia Baraza hilo kwa kutoa ruzuku ya shilingi Milioni 130 kila mwaka shughuli za uendeshaji wa baraza hilo kisiasa kiuchumi na kijamii.
Mbali na hayo, aliwaomba vijana kujiunga na baraza hilo na kushirikiana na serikali na wadau wa maendeleo, vijana kujipanga katika miradi ya kiuchumi.
Hata hivyo aliwasisitiza wajumbe kuchagua viongozi ambao watalisaidia baraza hilo liweze kusonga mbele kimaendeleo bila ya kuangalia dini, rangi wala kabila.
Nae Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Ayoub Mohammed Mahmoud, alisema vijana wafahamu kuwa muelekeo wa serikali ya awamu ya nane kwenye uchumi wa bluu na Viwanda ni fursa kwao.
Alieleza kuwa katika kutambua kuwa Zanzibar mpya inakwenda Kaskazini Unguja, kutokana na kuwepo kwa mradi mkubwa wa bandari ya Mangapwani anaozungumza fursa kama vijana kuliona hilo kwani ajira 300,000 ndio zitakazotoka katika mambo hayo.
Nao vijana hao walimpongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, kwa kuwateua vijana ambao jambo hilo limewapa ari kufanya kazi na kuahidi kuwa wataendelea kusimamia suala la amani, umoja na mshikamano wakisisitiza kuwa hawatokuwa na muhali kwa mtu yoyote ambae atataka kuichafua amani iliyopo.