Asema zinahamasisha umoja, udugu kwa watanzania

NA OTHMAN KHAMIS, OMPR

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema serikali za Tanzania, zitaendelea kuidumisha falsafa ya Mwenge wa Uhuru iliyolenga kuhamasisha kasi ya maendeleo ya kiuchumi na kudumisha umoja wa Watanzania.

Dk. Mwinyi alitoa kauli hiyo jana katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla wakati akizindua mbio maalum za Mwenge wa Uhuru zilizofanyika katika kiwanja cha Mwehe kilichopo Makunduchi Mkoa wa Kusini Unguja.

Alisema Mwenge wa Uhuru ulipoasisiwa ulizaliwa na falsafa ambazo zina umuhimu mkubwa kwa maisha ya watanzania ikiwemo kudumisha umoja, udugu na kuhamasisha maendeleo kwa Watanzania.

Alifahamisha kuwa dhamira ya serikali ya awamu ya sita ya muungano ni kuhakikisha Tanzania inakuwa na uchumi wa kati wa juu ifikapo mwaka 2050 kwa kuimarisha uwekezaji wa miradi ya kiuchumi.

Dk. Mwinyi alisema kwamba kwa lengo la kuchochea ukuaji wa uchumi kufikia uchumi wa kati wa juu na hatimae kuifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zilizoendelea, huku matumizi ya teknolojia ya habari yakipewa kipaumbele.

Alisema matumizi ya tehama yanaongezeka kwa wastani wa asilimia 8 kwa upande wa Tanzania bara kwa mwaka katika kipindi cha mwaka 2015 hadi 2019 na kusaidia mafanikio yaliyofikiwa.

Alibainisha kwamba wafanyabiashara na wananchi wengi wanafaidika na maendeleo ya sekta ya mawasiliano katika kuendesha maisha yao jambo ambalo limepunguza gharama za kuendesha biashara.

Dk. Mwinyi alitahadharisha kwamba wapo baadhi ya watendaji wanatumia vibaya mfumo wa Tehama kwa kujihusisha na uhalifu na vilivyo kinyume na maadili ya watanzania hali inayozua taharuki na kuhatarisha amani ya Taifa.

Aliendelea kuwakumbusha wananchi mahali popote walipo waendelee kuziunga mkono serikali zao ili yale malengo yaliyoainishwa ndani ya Ilani na Sera katika kuwahudumia Wananchi ziweze kufikiwa vyema.

Alizipongeza wizara zote mbili zinazosimamia shughuli za Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa kutoka serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kutimiza wajibu wao kikamilifu.

Akitoa taarifa ya mbio maalum za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2021, waziri wa Utalii na Mambo ya Kale, Leila Mohamed Mussa ambaye pia ni kaimu waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, alisema Mwenge wa Uhuru unawazindua wananchi juu ya umuhimu wa kupiga vita vitendo vya rushwa, dawa za kulevya na udhalilishaji.

Alielezea matumaini yake ya kufana kwa Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka huu kutokana na kazi kubwa iliyochukuliwa na viongozi na wataalamu katika kuwafinyanga vijana waliopewa jukumu la kutembeza Mwenge huo katika wilaya zote 150 za Tanzania ndani ya siku 150.

Kwa upande wake akitoa salamu za serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu-Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Jenista Joaquim Mhagama alisema mbio za mwaka huu zimeandaliwa maalum kufikia kikomo chake Mkoani Geita wilaya ya Chato ili kuheshimu mchango mkuu uliotolewa na Rais wa awamu ya tano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli.

Mhagama alisema mbio za Mwenge wa uhuru Tanzania zilizorejeshwa tena serikalini kwa zaidi ya Miaka 29 sasa zimekuwa zikiamsha ari na hamasa ya kuibuka kwa miradi ya Kiuchumi na Maendeleo katika maeneo mbali Nchini Tanzania bara na Zanzibar,

Mapema akitoa salamu za Mkoa Mwenyeji wa Kusini Unguja, Mkuu wa Mkoa huo Rashid Hadid Rashid alisema Mkoa huo umepata bahati ya Mwenge wa Uhuru kwa kuzinduliwa mara ya pili kutanguliwa na ule wa mwaka 2001 katika kijiji cha Mwera.

Mwenge Uhuru utakimbizwa katika wilaya 150 za Tanzania bara na Zanzibar na  zitafikia kilele mkoani Geita wilaya ya Chato mnamo Oktoba 14 mwaka huu, ambapo ujumbe wa mwaka huu unaeleza Tehama ni msingi wa Taifa Endelevu itumie kwa usahihi na Uwajibikaji.