Miradi mipya, iliyopitiwa miaka iliyopita kukaguliwa

Watajwa kuimarisha umoja mshikamano wa watanzania

NA MADINA ISSA

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa mbio za mwenge wa uhuru kitaifa unaofanyika leo mkoa wa kusini unguja.

Akitoa taarifa kwa waandishi wa Habari, Kaimu waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Lela Mohamed Mussa, alisema uzinduzi huo utafanyika katika uwanja wa Mwehe, Makunduchi ambapo viongozi wa kitaifa wa seriklai zote mbili ma Mabalozi wanaowakilisha nchi zao nchini watahudhuria.

Lela alieleza kuwa maandalizi shughuli hiyo yamekamilika ambapo kamati ya kitaifa na mkoa huo zimefanya kazi zilizopangiwa kwa mashirikiano makubwa chini ya wizara zinazohusika na maswala ya vijana za Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Aidha alisema, katika uzinduzi huo unatarajiwa kuwepo kwa wananchi zaidi ya 5,000 ambapo huduma mbali mbali zitakuwepo ikiwemo miundombinu zimekamilika katika hafla hiyo.

Aidha alisema kuwa kwa mwaka huu mkoa wa Kusini umepewa heshima a ya kuzinduliwa kwa mwenge huo, ikiwa ni mara ya pili katika historia za mwenge huo, hivyo aliwataka wananchi wa mkoa huo na mengine ya jirani kujitokeza kwa wingi na kuhudhuria katika tukio hilo.

“Watendaji wa serikali zote mbili wamefanya kazi usiku na mchana ili kuhakikisha uzinduzi wa mbio za mwenge unafanikiwa, hivyo nawaomba wananchi wajitokeze,” alisema Lela.

Nae, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu, Jenista Joakim Mhagama, alieleza kuwa huu ni mwaka wa 29 toka mbio hizo ziwe chini ya uratibu na usimamizi wa serikali.

Aidha alisema katika kipindi cha mbio hizo, miradi mbali mbali ya maendeleo itakaguliwa, kuwekewa mawe ya msingi na kuzinduliwa pamoja na kufuatilia miradi iliyozinduliwa katika mbio zilizopita.

“Tumeshuhudia mara nyingi miradi mingi inayozinduliwa na mwenge inakufa hivyo hawa viongozi walioteuliwa mwaka huu watapita katika miradi iliyozinduliwa ili kuona maendeleo yake,” alisema.

Hivyo, alisema ni vyema kwa watendaji waliokuwa na miradi hiyo kuendelea kuisimamia miradi hiyo na mradi wowote utakaobainika kutoendelea na kazi hatua stahiki zitachukuliwa dhidi yake.

Alisema kuwa toka kuasisiwa kwake, mwenge huo umewaunganisha Watanzania katika masuala mbali mbali yakiwemo kuimarisha mshikamano, kuendeleza umoja, amnai na utulivu.

“Kila mahali mwenge ulipofika iliacha ujumbe na watu wamekuwa wakijadili maendeleo, mshikamano wa kitaifa pamoja na namna ya kuimarisha uchumi bila ya kuangalia itikadi za siasa, dini na kikabila,” aliongeza Mhagama.

Mwenge wa uhuru uliasisiwa na kuanza kukimbizwa katika maeneo mbali mbali ya Tanzania bara na baadae Zanzibar mwaka 1961 ikiwa ni kielelezo cha uhuru na umoja wa watanzania na miongoni mwa tunu za taifa unatarajiwa kukimbizwa katika wilaya 150 ambapo kilele chake kitafanyika mkoani Geita, Oktoba 14 mwaka huu.

Pamoja na mambo mengine, katika mbio hizo, ujumbe mbali mbali unaohusiana na maswala ya maendeleo ya taifa na ustawi wa jamii Hivyo, alisema ni vyema kuwashukuru waasisi wa nchi, Mwalimu Juias ambapo kwa mwaka huu, mwenge huo utabeba ujumbe usemao; ‘Tehama ni msingi wa taifa endelevu, itumie kwa usahihi na uwajibikaji’.