NA RAJAB MKASABA, IKULU

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema serikali inaaendelea kuutafutia  uvumbuzi mgogoro wa kampuni ya Masterlife Microfinance Ltd, ili kuwasaidia waathirika waliowekeza fedha katika kampuni hiyo.

Dk. Mwinyi alieleza hayo jana ikulu jijini Zanzibar alipofanya mazungumzo na wawakilishi wa wananchi walioweka fedha zao katika kampuni hiyo iliyokuwa ikiendesha shughuli za kifedha kinyume na sheria na taratibu za nchi.

Alisema juhudi zinaendelea kuchukuliwa na serikali ikiwa pamoja na kukaa na uongozi wa kampuni hiyo ya Masterlife ambayo ilikushanya fedha nyingi za wananchi kinyume na taratibu za nchi ambapo fedha zilizopatikana kutoka kwa Kampuni hiyo hadhikidhi malipo kwa waathirika.

Dk. Mwinyi alisema kuwa taarifa zilizotolewa na uongozi wa Mastarlife ni watu  11,000 tu ambao wametoa fedha zao na sio watu 39,000 idadi iliyotolewa hapo mwanzo na maofisa wa Wizara ya Fedha.

Alisema kuwa kwa upande wake ana nia njema kwani ameapa kuwatendea haki wananchi wa Zanzibar na hayuko tayari kuona mwananchi yoyote anadhulumiwa.

Alisema angependa jambo hilo liishe kwa salama kwani anatambua kwamba ana dhima kubwa kwa wananchi wa Zanzibar na kueleza kuwa kilichokuwa kikifanyika sio mfumo wa ‘Musharakah’ kama ilivyoelezwa na bali uliokuwa ukifanyika ni mfumo wa  ‘Pyramid Scheme’.

Alisema kilichokuwa kikifanywa na kampuni ya Masterlife  hakikubaliki katika jamii na anaendelea na mazungumzo na kampuni hiyo katika kuhakikisha fedha za watu zinarudi kwani walioathirika ni wengi.

Alisema kuwa serikali haina nia ya mwananchi hata mmoja kuikosa fedha zake na kilichokuwepo ambacho ilipelekea serikali kuisimamisha kampuni hiyo ni kuona kwamba watu wengi wangejiunga na hatimae kukosa haki zao.

Alisema kwa kawaida hakuna biashara inayoweza kumpa mtu faida ya asilimia mia pale mwanzoni kwa miezi mitatu na hakuna faida inayoweza kumpa mtu faida ya asilimia 50 kwa miezi mitatu.

Alisema kuwa serikali haikuwa na nia ya watu wadhulumiwe ama wapoteze fedha zao kwani Kampuni hiyo haikuwa na biashara itakayotoa faida ya kuwapa watu.

Aliongeza kuwa biashara zilizokuwa zikiendeshwa na kampuni hiyo hazikuwa na lengo zuri la kutoa faida kwa watu na hata kiwango kinachotolewa cha watu waliojiunga na kampunin hiyo si cha uhakika.

Alisema kuwa anachotafuta hivi sasa ni kupata ufumbuzi kabla ya kuchukua hatua na ameahidi kulifuatilia suala hilo mpaka watu wapate fedha zao.

Alieleza kuwa azma ni kulifanyia kazi suala hilo na kusema kwamba uvamizi uliofanyika katika kampuni hiyo ulifanwya kwa lengo la kuhakikisha angalau kilichokuwepo kiweze kupatikana ambapo fedha zilizopatikana hazikufika hata bilioni 5 licha ya kukusanya fedha nyingi za watu.

Dk. Mwinyi alisema kwamba jambo hilo ni kubwa sana na watu waliochukuliwa fedha zao ni 11,000 ambao ni wengi sana licha ya idadi ya awali iliyotolewa na maofisa wa wizara kuwa ni watu 39,000, lakini hata hivyo ni watu wengi kwa Zanzibar.

Alisema kuwa taarifa aliyoitoa kwa wananchi Aprili 6 mwaka huu ni kwa ajili ya kuutahadharisha umma kutokana na mchezo huo mchafu uliokuwa ukifanywa na kampunin hiyo kwani kila mtu alikuwa anataka kupeleka fedha yake ambapo hali hiyo ingeachiwa ingeliathiri watu wengi zaidi.

Alisema miongoni mwa mambo aliyoyafanya ni kuviita vyombo vya sheria na kuwapa maelekezo ya kwamba ni vyema watu wa kampuni hiyo watafutwe wahusika ili wawalipe watu pesa zao kwanza na baadae mengine yafuate.

Dk. Mwinyi alieleza juhudi alizozichukua katika kuhakikisha taratibu za kifedha zinafanywa lakini akasisitiza ni kuhakikisha fedha hizo zinarudi na baada ya hapo ndio masuala mengine yatafuata kama vile ushauri.

Waathirika hao kwa upande wao walitoa shukurani zao kwa Dk. Mwinyi na kueleza jinsi walivyofarajika kutokana na maelezo na maelekezo yake juu ya suala hilo na kuzifahamu hatua zinazochukuliwa na serikali.